Kibali cha mazishi chapasua katikati familia ya mwanasiasa
MANDUGU wa mwanasiasa mmoja kutoka Kaunti ya Kisii, aliyekufa Aprili 19, 2023, wameapa kutokanyaga kwenye mazishi ya mwenzao Naftali Ontweka Onderi baada ya mke wake kuwashinda kwenye kesi kuhusu mahali pa kuzikwa kwa marehemu.
Kifo cha Bw Onderi aliyewahi kuwania ubunge wa Bomachoge Borabu mnamo Agosti 9, 2022, kimeibua mzozo kati ya nduguze na mjane wake, Bi Zipporah Masese Onderi.
Huku mkewe na wanawe wakitaka wamzike katika makazi yake ya kifahari, yaliyoko eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos, nduguze wanasema ni lazima wamzike kaka yao kijijini Kiango, Kisii.
Siku chache kabla ya nduguze kutaka kumzika Kisii, Bi Zipporah alienda kortini na kupata kibali cha kuzuia mazishi hayo.
Kabla ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu kumpa afueni Bi Onderi kuwa mumewe anafaa kuzikwa katika eneo la Kamulu, mahakama ya hakimu, ambapo kesi hiyo ilianzia, ilikuwa imesema kwamba Onderi anafaa kuzikwa katika Kaunti ya Kisii.
Tangu mjane huyo apate agizo la kumzika mumewe katika shamba lake la Kamulu, mpasuko mkubwa umetokea baina ya pande hizo mbili.
Uhusiano wao umeingia doa kabisa ambapo sasa ndugu zake marehemu wameapa kutojihusisha na mazishi hayo.
“Sisi hatutakanyaga Kamulu. Kesi hiyo imekwisha na ikiwa shemeji yetu aliamua hivyo ndivyo anataka, basi na iwe,” Joseph Ontweka, kakake mkubwa marehemu alisema.
Aliongeza kuwa watafanya mipango ya kulifunika kaburi walilokuwa wamechimba ‘kumpumzisha’ ndugu yao bila kufuata tamaduni zozote.
“Tutafanya ibada siku ile ile watakayokuwa wanafanya mazishi ya ndugu yetu Kamulu,” Mogusu Ontweka, kaka mwingine wa marehemu aliongeza.
Mzee huyo alizungumzia kisa cha ng’ombe mmoja aliyeanguka ndani ya kaburi hilo walilokuwa wamemchimbia ndugu yao na akadai kitendo hicho kilituma ujumbe mkali ambao hakufafanua zaidi.
Baada ya ushindi alioupata Bi Onderi, mjane huyo alisema alikuwa amepokea simu kutoka kwa Wakenya wengi waliokuwa wakipitia migogoro kama yake na akasema walimweleza kuwa sasa wamepata mahali pa kuanzia.
Bi Onderi hata hivyo, kwenye mahojiano na Sunday Nation alisema milango ya kuingia kwake Kamulu iko wazi kwa yeyote atakayetaka kuhudhuria mazishi ya mumewe.
Mwili wa marehemu ungali katika hifadhi ya maiti ya Lee. Marehemu anajulikana vyema nyumbani kwao Kiango kwa kujitolea kwake kufanya kazi za kuinua jamii.