Habari Mseto

Kibwana apinga mageuzi ya Katiba

November 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PIUS MAUNDU

SIKU moja baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kuandaa mkutano na magavana ili kupata muafaka kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), Gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana amedai kwamba katiba ya sasa haifai kufanyiwa mabadiliko.

Prof Kibwana alikashifu serikali kwa kutotekeleza katiba ya sasa vilivyo tangu irasimishwe mnamo 2010. Alitaja ukiukaji wa katiba mara kwa mara kupitia asasi ya bunge na afisi ya Rais hasa akirejelea kucheleweshwa kwa mgao wa kaunti kila mwaka wa kifedha.

Kauli ya Prof Kibwana inashangaza kwa kuwa siku za nyuma, amekuwa kati ya wanasiasa waliokuwa katika mstari wa mbele kurindima ngoma ya BBI hasa katika kaunti za Ukambani.

“Serikali inafaa kwanza ihakikishe kuwa katiba ya sasa inatekelezwa ipasavyo kabla ya kushiriki mchakato wa kuitaka ibadilishwe,” akasema Prof Kibwana akisisitiza uanaharakati wa zaidi ya miaka 20 uliosababisha hata vifo vya wanasiasa haujazaa matunda yoyote katika utekelezaji wa mabadiliko waliyoyapigania.

Aidha gavana huyo alishangaa kwa nini ripoti ya BBI inalazimishwa kwa raia badala ya mashauriano kukumbatiwa na muafaka unaoridhisha viongozi wa mirengo yote uafikiwe. Kauli sawa na hiyo imekuwa ikivumishwa na Gavana wa Machakos, Dkt Alfred Mutua.

Hata hivyo, pingamizi za magavana hao wawili wanaohudumu muhula wao wa mwisho, sasa unadaiwa kuchochewa na hatua ya Kinara wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka kujiweka kama msimamizi wa kampeni za BBI katika eneo zima la Ukambani.

Mwaka jana, Bw Musyoka na magavana hao wawili walitofautiana hadharani kuhusu aliyepaswa kusimamia kampeni za BBI eneo hilo. Prof Kibwana na Dkt Mutua walisisitiza kuwa walikuwa katika nafasi nzuri ya kuendesha kampeni hizo kwa kuwa wako karibu na wananchi waliowachagua.

Bw Musyoka naye aliona njama hizo kama nia ya kudidimiza umaarufu wake ndipo akaandaa mkutano mkubwa na wabunge, maseneta na madiwani wa Wiper ambapo alisema atasimamia kampeni hizo.

Hata hivyo, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Makueni, Bi Rose Museo ambaye ni mwandani wa Bw Musyoka, alitoa wito kwa pande zote kuungana kwa kuwa BBI itabadilisha pakubwa maisha ya jamii ya Akamba.

“Hali ya sasa ambapo wanasiasa vigogo wa jamii mbalimbali na viongozi wenye vyeo vya juu ndiyo wanahusika na masuala ya BBI, kunasawiri ripoti hiyo kama si ya mwananchi wa kawaida,” akasema Dkt Mutua kwenye mkutano wa umma jijini Mombasa mwezi Oktoba.

“Tunataka mchakato wa BBI uwahusu wote jinsi ilivyokuwa kwenye Kongamano la Bomas ambapo wanasiasa, viongozi wa kidini, wafanyabiashara kutoka sekta ya kibinafsi, vijana na viongozi wa kijamii wanahusishwa na maoni yao kujumuishwa,” akaongeza Dkt Mutua.