• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Kicheko mshukiwa kutetemeka huku jasho la kizimbani likimtiririka

Kicheko mshukiwa kutetemeka huku jasho la kizimbani likimtiririka

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa wizi wa Sh49 milioni kutoka benki ya Sidian Jumatano alichekesha watu mahakamani alipofichua hajawahi kukamatwa ama kushtakiwa kwa sababu ya wizi.

Akasema Geoffrey Nyamari aliposhtakiwa, “Tangu nizaliwe sijawahi kukamatwa ama kushtakiwa. Hii ndiyo mara yangu ya kwanza kufikishwa kortini. Haki nimeshtuka hakimu.”

Huku akitetemeka na kutokwa na kijasho chembamba, Nyamari alimweleza hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot , “Haki mheshimiwa sijawahifikishwa kortini mbeleni. Naogopa sana. Hata sijawahi hata kuiba.”

Hakimu alimweleza mshtakiwa kwamba kile anatakiwa kufanya ni kutulia kisha aombe dhamana.

“Eti unasema nini mheshimwa?” Nyamari alimwuliza hakimu.

Bw Cheruiyot alimfafanulia kwamba atamwachilia kwa dhamana ndipo afanye kesi akiwa nje.

Kiongozi wa shtaka Bw Kennedy Panyako hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Mahakama ilimpa dhamana ya Sh5 milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Hakimu alimweleza ikiwa atashindwa kulipa dhamana hiyo anaweza kulipa pesa tasilimu Sh1.5 milioni pesa tasilimu.

Mshtakiwa alikabiliwa na shtaka kwamba kati ya Januari 1 na Machi 1 mwaka huu mahali pasipojulikana humu nchini akishirikiana na watu wengine walidukua kwa njia ya mitandao akaunti za watu na kuiba Sh49,387,000.

Shtaka mbadala lilisema alipatikana ameweka katika akaunti yake Sh1,280,000 akijua zimepatikana kwa njia isiyo halali ama zimeibwa.

Mshtakiwa alitiwa nguvuni Machi 5 na kufikishwa mahakamani Machi 6, 2019.

Kesi itatajwa baada ya wiki mbili.

You can share this post!

Uhuru atakiwa apuuze Ajenda 4 Kuu ili kuzima ufisadi kwanza

Gor Mahia yatulia Misri ikisubiri marudiano na Zamalek

adminleo