Kidero alia EACC ilimnasa kimakosa
Na COLLINS OMULO
ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Evans Kidero ameishambulia Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) akiisuta kwa kile alichosema ni hatua yake ya kumhukumu “katika mahakama ya umma”.
Akiongea jana akiwa katika kizuizi cha polisi kwa njia ya simu Dkt Kidero alisema kushikiwa kwake kila mara kunaongozwa na nia mbaya ni shughuli ya uhusiano mwema ambao haiwezi kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.
Gavana huyo wa kwanza wa Nairobi alikamatwa Ijumaa pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Wafanyakazi katika serikali yake George Wainaina. Hii ni baada ya EACC kufanya uchunguzi kufunguza sakata ya malipo ya Sh68 milioni na Serikali ya Kaunti ya Nairobi kwa kampuni moja ya wanasheria.
Dkt Kidero alishangaa ni kwa nini alikuwa akikamatwa Ijumaa kwa makosa ambayo yalitendeka miaka mitatu kabla yake kuchaguliwa gavana wa Nairobi.
Alilamikia kile alichodai kuwa dhuluma aliyotendewa na wapelelezi wa EACC akisema walifika nyumbani kwake saa kumi alfajiri kumkamata ilhali watuhumiwa wenzake hawakamatwa jinsi hiyo.
“Maafisa wa EACC walifika nyumbani kwangu saa kumi alfajiri kunikamata. Walinifikisha katika makao makuu yao saa moja asubuhi na nikawapata kundi na wanahabari wa humu nchini na kimataifa tayari kupeperusha habari hizo.
“Wakati huo washukiwa wengine walikuwa manyumbani mwao na hawakuwa na habari kwamba walikuwa wakisakwa. Baadaye walipata habari kupitia vyombo vya habari wakishauriwa kujiwasilishwa kwa hiari,” Dkt Kidero akasema.
Na akauliza ni kwa nini EACC ilimkamata alfajiri lakini haikumwasilisha kortini moja kwa moja ili afunguliwe mashtaka ambapo ushahidi wa kumhusisha na uovu huo ungetolewa na kuthibitishwa.
Dkt Kidero alishangaa ni kwa nini kesi dhidi yake inapewa uzito zaidi kulika sakata zingine za thamani ya mabilioni ya fedha, zikiwemo ununuzi wa vifaa vya matibabu, sakata za ujenzi wa mabwawa na zingine nyingi. Alisema kesi hizo zimechunguzwa lakini washukiwa hawajawasilishwa kortini hadi sasa.
“Hii ni ithibati tosha kwamba haja kuu ya tume hii ni kujipendekeza kwa vyombo vya habari na kunihukumu machoni pa umma. Nilikamatwa saa kumi alfajiri, mbona sikupelekwa kortini siku hiyo. Inaonekana hii ilikuwa ni njama ya kuzuilia katika kituo cha polisi wikendi mzima,” akaeleza.