Habari Mseto

KIFO KISIMANI: Majonzi, uchungu mtoto wa miaka 2 akifa maji kwenye kisima

Na OSCAR KAKAI October 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKATI Alice Limareng alipoamka mapema asubuhi Ijumaa, hakujua kuwa dakika chache baadaye atampoteza mwanawe mvulana mpendwa mwenye nguvu wa umri wa miaka miwili.

Masaibu yalimkumba mama huyo baada ya mwanawe kuanguka kwenye kisima ambacho kiko mita tatu kutoka kwa nyumba yao.

Malaika huyo Fabion Korir ambaye ni mtoto wa tatu kwenye familia anasemekana kuamka mapema, mwenye nguvu na kuanza kucheza kama kawaida yake.

Mkasa huo umewaacha wakazi wa kijiji cha Matopeni, eneo la Murkwijit, Kaunti ya Pokot Magharibi kwenye majonzi, hofu na uchungu.

Mamake ambaye anajulikana kama “Mama Korir” amekuwa kwenye mshutuko na hajaongea tangu tukio hilo litokee.

Babake Allan Limareng ambaye ni mwanajeshi hakuwa nyumbani wakati wa tukio hilo.

Kulingana na familia, mamake mtoto huyo alifungua kisima hicho asubuhi mapema akachota maji sababu kuna watu walikuwa waje kuosha kisima hicho.

Kisima hicho chenye futi 35 kilisalia kuwa wazi kikingojea watu wa kukisafisha.

Mama huyo alirudi kwenye nyumba na kwa bahati mbaya bila kujua mtoto alisongea kwenye kisima na kuanguka ndani.

Hii ililazimu mama huyo kupiga kamsa na kuwapasha habari wanakijiji  ambao walifika kwa wingi kushuhudia mkasa huo.

Mjomba wake mvulana huyo Abraham Cheruyoit ambaye aliongea na vyombo vya habari anasema kuwa bado hawajaamini kuwa mtoto huyo hayupo tena akisema kuwa alikuwa mcheshi na alionyesha dalili za kuwa na ndoto nzuri maishani.

“Kifo chake ni pigo kuu kwetu wakati huu mgumu. Dada yangu amechanganyikiwa na akaa tu msituni. Hatujui la kufanya. Kijana huyo alikuwa tumaini kwa familia,” alisema.

“Tumevunjika mioyo kuwa mtoto wa dadangu ameaga akiwa mdogo,” alisema.

Scholar Kapello, mshirikishi wa shirika la Msalaba Mwekundu kwenye kaunti hiyo anasema kuwa ilikuwa Ijumaa yenye huzuni ambayo iliacha kila mtu na mshutuko.

Alisema kuwa walifaulu kuondoa mwili huo kutoka kwenye kisima baada ya masaa kadhaa.

‘Tulimpata mama akilia sana na tukampa huduma ya kwanza na kumliwaza. Mtoto alikuwa tayari amekufa na tukaita maafisa wa kukabiliana na majanga,” alisema.

Aliwaonya wakazi akisema kuwa visa vya watu kufa kwenye visima vimeongezeka katika eneo hilo.

“Tunataka wakazi wawe makini na visima. Tumekuwa na visa vingi vya watu kufariki kwenye visima. Wale wanatumia visima wanafaa kuchukua tahadhari. Tutaanza mpango wa kuhamasisha wakazi ili wajiepushe na visa kama hivi.  Ni makosa kupoteza watoto wadogo kama hao kwenye mikasa kama hiyo,” alisema.

Haya yanajiri huku visa vya watu kufariki kwenye visima vikiwa vingi katika eneo hilo.

Mei mwaka huu, watu wawili walifariki ndani ya kisima cha mita 50 katika boma katika mtaa wa mabanda wa Mathare, eneo la Lityei, mjini  Makutano, Kapenguria baada ya watu hao kujaribu kuondoa ndoo na kamba ambazo zilikuwa zimeanguka ndani ili walipwe Sh200.

Mwaka jana, watu wawili walifariki kwenye kijiji hicho ndani ya kisima.

Miaka miwili iliopita, wanafunzi watatu walifariki baada ya kuanguka kwenye kisima kwenye shule ya msingi ya Chewoyet.

Mwili wa mtoto huyo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Kapenguria.

[email protected]