Kijana aliyepigwa na kumwagiwa asidi na polisi hatarini kukatwa miguu
KIJANA mmoja, mwanafunzi wa kidato cha pili yupo katika hatari ya kukatwa miguu baada ya kupigwa vibaya na polisi kwa tuhuma za kuiba vipuri vya tingatinga.
Felix Senet Takona, 17, alikamatwa Oktoba 10, 2025 katika Kituo cha kibiashara Naroosura Kaunti ndogo ya Narok Kusini.
Wiki mbili baadaye, dogo huyo anapambana kusalia hai katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok baada ya kupigwa na polisi na kujeruhiwa akiwa kuzuizini.
Madaktari katika hiyo wamefichua kuwa majeraha ambayo anayo ni mabaya zaidi na huenda ikabidi mguu wake ukatwe ili kuyaokoa maisha yake.
Akiongea akiwa hospitalini ambako amewekewa pingu mkononi huku akilindwa na polisi, Felix alifichua kuwa alipigwa kwa nyororo kisha kumwagiwa kemikali anachoshuku ni asidi miguuni.
Alimwagiwa kemikali hiyo akiwa katika kituo cha polisi cha Naroosura baada ya kukamatwa kwake.
“Nilikamatwa saa nane mchana mnamo Oktoba 10 katika kituo cha kibiashara cha Naroosura. Nikiwa kuzuizuni polisi wawili walinifunga kwa minyororo wakanipiga na kunijeruhi ili nikiri makosa ambayo sikuyatenda,” akaambia Taifa Leo.
“Walinimwagia asidi miguuni na kukataza familia yangu isinifikie. Nilipigwa kila usiku nikiwa kizuizini na walikuwa wakiniambia nikubali mashtaka dhidi yangu ama waniue,” akasema akiwa hospitalini.
Alihamishwa hadi kituo cha polisi mnamo Oktoba 12. Taifa Leo imebaini kuwa alipofikishwa mahakamani mnamo Oktoba 13, nakala ya mashtaka ilibadilishwa kutoka kuiba vipuri vya tingatinga hadi kuingia kwenye jengo na kuiba.
Baada ya kufikishwa mahakamani, hakimu aliamrisha apelekwe hospitali ili atibiwe kabla ya mashtaka dhidi yake kuwasilishwa rasmi ili ayakanushe au kuyakiri.
Siku iliyofuata alifikishwa kortini na akashtakiwa kwa kuvunja duka katika kituo cha kibiashara cha Naroosura na kuiba lita 10 ya mafuta ya kupikia yenye thamani ya Sh2,500 pamoja na pesa taslimu Sh34,000.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Narok Riko Ngare alisema polisi wanachunguza kisa cha kijana huyo kwa lengo la kubaini ukweli.