Habari Mseto

Kijana atumia mabaki ya mbao kuunda viti vya maana

April 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

NA RICHARD MAOSI

[email protected]

Kampeni ya kupiga marufuku ukataji miti kiholela chini ya mwavuli wa UNEP, inaendelea kushika kasi kote ulimwenguni, huku mabalozi wa kuyalinda mazingira dhidi ya uharibifu wakivalia njuga swala hili.

Isitoshe agizo la kufunga maeneo yenye misitu, uchomaji wa makaa, kuchanja na kuuza kuni ikiwa ni hatua ya pili kuziba mianya ya kuangusha miti.

Kwingineko mafundi wanaotumia mbao kutengeneza bidhaa kama vile meza, viti, makabati na vitanda wakilazimika kusaka njia mbadala ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku mara tu baada ya kuachana na biashara ya mbao.

Hizi zikiwa ni baadhi ya harakati za kuhakikisha kuwa Kenya inafikisha asilimia 10 ya misitu, ifikapo 2030 na kuendelea kwa mujibu wa wizara ya mazingira, na kanuni za umoja wa mataifa.

Lakini hali ni tofauti kwa kijana Samwel King’ori mwanafunzi wa mwaka wa mwisho kutoka taasisi ya Sayansi na kiufundi ya Rift Valley Institute of Science and Technology(RVIST) .

Samwel anaweza kutengeneza vyombo vya thamani kutokana na mabaki ya miti iliyokatwa zamani iliyoharibika almaarufu kama visiki, ambavyo mara nyingi havina kazi mara tu baada ya mti kung’olewa.

Kulingana naye ana ujuzi wa kugeuza visiki hadi vikawa, maumbo mbalimbali ya kependeza au vyombo adhimu mfumo unaofahamika kama Natural Wood Design ambao alijifunza tangu mwaka wa 2011 alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Tangu mwaka wa 2017 alipokamilisha masomo ya shule ya upili alipata changamoto ya kujilipia karo kwa sababu alikuwa akitokea kwenye familia yenye kipato kidogo.

Akajiwekea malengo kuwa ni lazima angekuja kuelimika katika taasisi ya kiufundi jambo lililomfanya atafute mbinu ya kujilipia karo.

Mbali na kutafuta vibarua kila mahali mjini Nyahururu ambako alizaliwa hakufanikiwa kupata kazi ya kudumu kwa sababu mara nyingi vibarua vilikuwa vya muda mfupi, na malipo yalikuwa ni duni.

Ndiposa akaamua kujiajiri na kuajiri vijana wengine akiamini kuwa, bidii na msukumo wa ndani ndio chanzo cha mafanikio kwa binadamu yeyote anayelenga kufika mbali.

“Nilihitaji mtaji kidogo mwanzoni wa 3500 , katika hatua za kwanza kabla ya kujistawisha katika shughuli hii ambayo ninategemea kila siku,”akasema.

Alieleza kuwa hii ni kazi kama ile ya ofisini kwa sababu, kipato chake kimemsaidia kujianzishia miradi ya kujiendeleza kama vile ukulima na ufugaji kwao kijijini, mbali na kazi yake ya Natural Wood design.

Samwel anasema kuwa wateja wake wengi ni wanafunzi wenzake, walimu na wapita njia ambao mara nyingi hupendelea kununua bidhaa zake kutokana na hali ya juu ya ufundi.

Aidha anasema kuwa vyombo vyake vya samani kama vile viti na meza ni dhabiti na bei yake ni nafuu kwa raia wa kipato cha chini.

Kulingana naye amekuwa akiweka baadhi ya bidhaa zake mtandaoni ili kuwavutia wanunuzi wa kigeni ambao wanaweza kumsaidia kujiongezea kipato.

“Bidhaa zangu mara nyingi zinagharimu baina ya 500-60,000 ikiwa ni pamoja na meza, kabati na vitanda vya kisasa ambavyo haviwezi kupatikana katika maduka ya kijumla,”aliongezea,

Samwel mara nyingi huchukua siku mbili kutengeneza bidhaa nyepesi kama vile meza na viti , na takriban wiki nzima kuunda kitanda cha bei ghali hadi kikakamilika.

Aliongezea kuwa ili kutengeneza bidhaa za hali ya juu kama fundi anajifunza mitindo mbalimbali kutoka kwa wale ambao wamebobea

Hivi sasa analenga kuanza kutumia mtandao wa kijamii kama vile Facebook na Twitter ili kufikia soko la kimataifa, huku akiamini kuwa fursa hii itasaidia kuwaajiri vijana wengi hasa wakati huu Kenya inapopambana na hali ngumu ya Maisha wakati wa kuongeza nafasi za ajira miongoni mwa vijana katika ajenda yake kuu ya kukwamua uchumi.

Aliongezea kuwa kazi yake hunoga akiwa katika likizo maana hapo ndipo yeye hupata muda wa kutosha ili kuwatengenezea wateja wake bidhaa.

Aidha ndio mua anaotumia kupata maagizo mengi na kuyatumikia kwa wakati hususan msimu wa Krismasi na sherehe za mwisho wa mwaka wakati ambapo aghalabu huwa anatengeneza hela nzuri.

Anawashauri vijana kufanya kazi yoyote bila kuchagua endapo wanalenga kuja kuwa wajasiria wali wa kujitegemea siku za usoni.