Habari Mseto

Kijana Ian anajutia kosa la kumshambulia afisa

June 16th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

IAN Njoroge, barobaro mchanga aliyegonga vichwa vya habari mapema mwezi huu (Juni 2024) alipomcharaza afisa wa polisi kando ya barabara ya Kamiti, eneobunge la Roysambu, Nairobi hatimaye ameomba msamaha kwa serikali, afisa huyo na Wakenya.

Katika kisa hicho cha Jumapili, Juni 2, 2024, mvulana huyo alionekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni akimshambulia kwa makonde na mateke afisa huyo wa kitengo cha trafiki aliyetambuliwa kama Jacob Ogendo.

Lakini baada ya kukamatwa, kushtakiwa na kuachiliwa huru kwa dhamana, Njoroge, 19, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kiufundi Kenya (TUK) sasa anajutia kosa hilo huku akiahidi kutolirudia.

“Nachukua fursa hii kuomba msamaha kwa serikali, Idara ya Polisi na afisa Jacob Ogendo. Najutia na sitafanya kosa kama hilo tena,” anasema kwenye video akiwa afisini mwa aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko.

Katika video hiyo ambayo imepakiwa kwenye akaunti ya Sonko ya mtandao wa X (zamani Twitter) Ian anaonekana akiwa amevalia “Jamper” ya rangi ya samawati huku mkono wake wa kushoto ukiwa umefungwa bandeji.

Alikuwa ameandamana na wazazi wake, ambao hawakufichua majina yao na ambao pia waliomba msamaha kwa Bw Ogendo, 55, polisi na Wakenya kwa ujumla.

Aidha, Bw Sonko alitoa ombi sawa na hilo la msamaha akiahidi kugharamia matibabu ya Ian katika Hospitali ya Nairobi Womens, Nairobi.

Wiki jana, Hakimu Mkuu wa Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, Ben Ekhubi alimwachilia huru Ian kwa dhamana ya Sh700, 000 baada ya kutupilia mbali ombi la upande wa mashtaka kwamba aendelee kuzuiliwa.

Mvulana huyo alishtakiwa kwa makosa ya kumshambulia na kumjeruhi Bw Ogendo na wizi wa kimabavu.