Kikao cha kumng'atua Obado chatibuka
RUSHDIE OUDIA na IAN BYRON
MADIWANI katika Kaunti ya Migori, Jumanne waliahirisha kikao kilichotarajia kuwasilishwa kwa hoja ya kumng’atua mamlakani Gavana Okoth Obado, ikidaiwa walihofia uenezaji wa virusi vya corona bungeni.
Hatua hiyo ilijiri saa chache baada ya taharuki kutanda malori yaliyojaa polisi wa kupambana na fujo yalipotumwa kuzima ghasia endapo zingezuka.
Spika wa bunge la kaunti hiyo Boaz Okoth aliahirisha kikao baada ya kubainika kwamba hakukuwa na mipango ya kuhakikisha umbali baina ya mtu na mwingine miongoni mwa madiwani.
Madiwani wote 57 walikuwa wamehudhuria kikao cha Jumanne kabla ya kuahirishwa.
Hata hivyo, Bw Obado alisema atakubali uamuzi wa madiwani hao iwapo watafaulu kumuondoa ofisini.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Obado alisema kwamba hakuna mkutano ulioandaliwa kujadili au kupitisha kuwa aondolewe ofisini.
Alisema kwamba mtu mmoja au watu wawili hawawezi kudai kwamba wana kipimo cha uaminifu wake kwa chama cha ODM.
“Ninawaambia maafisa wa chama watoe maazimio ya mkutano wa kamati kuu ya chama iliyopitisha niondolewe ofisini. Iwapo nitaondolewa ofisini, naomba Mungu anipe amani ya kuendelea na ukulima na kazi zangu za juakali,” alisema Bw Obado.
Alisisitiza kwamba amekuwa mwaminifu kwa chama cha ODM licha ya njama za baadhi ya viongozi kumhangaisha.
Wiki jana, Mwenyekiti wa chama cha ODM John Mbadi na Katibu Mkuu wa chama Edwin Sifuna walikutana na madiwani 41 wa bunge la Kaunti ya Migori ambapo iliamuliwa kwamba gavana Obado aondolewe ofisini.