Kikundi chajitolea kuwahamasisha madereva kuhusu kanuni na sheria za trafiki
Na LAWRENCE ONGARO
KUFUATIA ajali za barabarani za kila mara katika Thika Superhighway, kikundi kimoja miongoni mwa wakazi wa Thika, kimejitolea kuhamasisha madereva umuhimu wa kufuata kanuni na sheria za trafiki.
Kikundi hicho likiongozwa na Bw Fredrick ‘Kinyambi’ Giturwa, kinaeleza kuwa ni muhimu kuhamasisha madereva kuhusu sheria za trafiki kwa sababu wengi wao hawatilii maanani sheria hizo.
“Sisi kama wazalendo tumejitolea kwa kutoa mwito wa ‘Keep Left Unless Overtaking & I suport Safe Driving’ tuliamua kuanza kuwapa madereva mwongozo mwema kwa sababu kuna mambo madogomadogo yanayopuuzwa kila mara,” alisema Bw Giturwa.
“Kwa siku za hivi karibuni tumeshuhudia ajali kadhaa katika Thika Superhighway, lakini tukichunguza kwa kina tunapata ya kwamba ni mambo madogo tu yanayopuuzwa na kuishia kusababisha ajali hizo,” alisema Bw Giturwa.
Alisema iwapo kila mmoja atachukua jukumu lake ipasavyo, ama awe ni dereva au mpitanjia, bila shaka ajali nyingi zitaepukwa kwa kiwango kikubwa.
Alisema yeye na marafiki wake wachache waliketi chini na kuamua kuwapa mafunzo machache madereva kwa kuwazungumzia kuhusu changa moto za ajali na jinsi ya kukabiliana nazo.
Alisema madereva wengi huendesha magari kwa kasi bila kuelewa jinsi ya kupishana na magari mengine na iwapo wangekuwa makini bila shaka ajali zingekuwa chache.
Hongo
Bw James ‘Jaymo’ Ng’ang’a, ambaye ni bloga wa mitandao ya kijamii mjini Thika aliwashutumu madereva wa matatu kwa kuzoea kutoa hongo kwa polisi.
“Iwapo madereva hangetoa hongo kwa Polisi hatungesema maswala ya hongo. Kwa hivyo kila mmoja akubali kufuata sheria ili mambo yaende sawa,” alisema Bw Ng’ang’a.
Alisema pia iwapo kutakuwa na nidhamu barabarani, bila shaka ajali nyingi zinazoshuhudiwa zitakuwa zitapungua pakubwa.
Naye Bw Mungai Ngige ambaye ni katibu wa chama cha walimu cha Knut alisema kila mdau anafaa achukue jukumu ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.