Habari Mseto

'Kilele cha maambukizi ya Covid-19 kushuhudiwa Agosti na Septemba'

May 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WIZARA ya Afya imetahadharisha kwamba Kenya itashuhudia kiwango cha juu zaidi cha maambukizi ya virusi vya corona katika miezi ya Agosti na Septemba.

Akiongea nje ya makao makuu ya wizara hiyo katika Jumba la Afya, Nairobi, kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt Patrick Amoth amesema huenda Kenya ikaanza kuripoti visa 200 vya maambukizi ya virusi vya corona kila siku.

“Upeo wa juu wa maambukizi utakuwa katika miezi ya Agosti na Septemba,” amesema.

Ametoa wito kwa Wakenya kuendelea kuzingatia maagizo yaliyowekwa, akisisitiza kuwa idadi ya visa vya maambukizi itaendelea kupanda sambamba na ongezeko la idadi ya watu wanaopimwa.

“Ni ombi letu kwamba sisi sote nchini tuendelee kuzingatia masharti haya kwa sababu yamehakikisha kuwa hospitali zetu hazilemewi,” Dkt Amoth akasema, akiongeza kuwa masharti hayo yamedumaza kuenea kwa virusi vya corona.

Mnamo Machi 2020 Serikali ilibashiri kuwa huenda Kenya ingeandikisha angalau visa 10,000 vya maambukizi ifikapo mwishoni mwa Aprili.

Lakini sasa, Dkt Amoth anasema masharti ambayo serikali iliweka wakati huo, kama vile kufungwa kwa shule na kufungwa kwa Nairobi na Mombasa, yalipunguza kusambaa kwa virusi vya corona kwa kiwango kikubwa.