• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Kilio kijijini Karibaribi wezi wakilenga wenye maduka, wafugaji

Kilio kijijini Karibaribi wezi wakilenga wenye maduka, wafugaji

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Karibaribi kilichoko Mang’u katika Kaunti ya Kiambu wanatoa wito kwa serikali kutuma polisi katika eneo hilo kushika doria na kuwakamata wezi wanaoiba mali na kuchangia kuzorota kwa usalama.

Kulingana na wakazi hao, wezi wamegeuza eneo hilo kuwa mawindo yao kwa kipindi cha mwezi mmoja mfululizo.

Inadaiwa kuwa wezi hao ni genge la watu kadha ambao wamejihami kwa silaha hatari huku wakitumia pikipiki kutekeleza uhalifu huo.

Wezi hao wanalenga sana maboma ya wakazi wenye mifugo na wale wenye maduka.

Uchunguzi uliofanywa umebainisha kuwa asilimia 80 ya wakazi ni wahasiriwa wa uhalifu huo ambao hutekelezwa sana usiku.

Kwa muda sasa, wakazi wamelazimika kujipanga kwa vikundi viwili ili kuweka doria usiku.

Mwathiriwa mmoja, Bi Wahito wa Kariuki, alisema mnamo Jumatatu usiku kondoo wake wapatao 10 waliibwa usiku wa manane.

“Tunashuku kwamba wezi hao wanapulizia wakazi dawa kupitia kwa madirisha kabla ya kutekeleza uhalifu huo,” alisema Bi Kariuki.

Alitoa wito kwa serikali kuingilia kati kwa sababu hayo yakiendelea, wezi watawageuza wakazi hao kuwa maskini.

Mkazi mwingine, Bw Wanjaria Njararuhi, alisema licha ya wakazi hao kufanya mikutano ya kiusalama bado hakuna jambo muhimu limeweza kufanikiwa.

“Wakazi wa hapa sasa wamezamia kujipanga kwa makundi mawili ili kupiga doria usiku,” akasema Bw Njararuhi.

Aliongeza kwamba wakazi wa eneo hilo kuingiza mifugo ndani ya nyumba ili kuepuka wizi huo usioeleweka.

Naye mmiliki wa duka mojawapo katika eneo hilo, Bw Zacharia Munyambu, alisema kuwa hivi majuzi duka lake lilivamiwa na wezi hao baada ya wahalifu hao kutolea mkewe na mlinzi vitisho.

“Waliwafunga hawa watu wawili–mke wangu na mlinzi– kwa kamba pamoja kabla ya kuchomoa fedha zilizokuwa kwenye sefu,” alisema Bw Munyambu.

Mnamo Jumatatu wakazi hao walifanya mkutano wa dharura huku wakiitaka serikali kuingilia kati haraka iwezekanavyo.

  • Tags

You can share this post!

Kanini Kega: Kuna mkono fiche unaomfadhili Nyoro kumpiga...

Pigo kwa Kingi vigogo wa PAA wakirudi ODM

T L