• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Kinara wa benki, mbunge na mkewe taabani kwa wizi wa Sh1 bilioni

Kinara wa benki, mbunge na mkewe taabani kwa wizi wa Sh1 bilioni

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mwenyekiti wa benki iliyowekwa chini ya mrasimu na Benki Kuu ya Kenya (CBK), Mohammed Zafrulla Khan, Mbunge wa Kibwezi Magharibi Bw Patrick Musimba , mkewe Angela Mwende na washukiwa wengine saba Alhamisi walishtakiwa kuibia benki hiyo zaidi ya Sh1.15 bilioni.

Kati ya kumi hao ni Bw Khan tu, aliyefika kortini kama walivyoamriwa na mkurugenzi wa jinai DCI Geoffrey Kinoti Jumatano wajisalimishe mahakamani.

Hakimu mkazi mahakama ya Milimani Bi Hellen Onkwani alitoa kibali cha kuwatia nguvuni washtakiwa hao.

Bi Onkwani aliagiza Polisi wawakamate na kuwafikisha mahakamani washtakiwa hao.

Walioagizwa wakamatwe ni Bw Musimba, mkewe Angela Mwende, Lucien Sunter, Ronald Petrus Vlasman na wawakilishi wa kampuni za Porting Access Limited na Itecs Limited.

Wakili Cecil Miller (pichani) anayemwakilisha Bw Khan aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema anaugua maradhi ya moyo .”

“Bw Khan anakabiliwa na kesi nyingine mbili na ameachiliwa kwa dhamana ya Sh2milioni pesa tasilimu. Naomba hii mahakama imruhusu ategemee dhamana hizo katika kesi hii,” alirai Bw Miller.

Ombi hilo lilipingwa na kiongozi wa mashtaka Bw Warui Mungai akisema ameagizwa na mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji aombe korti iwaachilie washtakiwa kwa masharti mapya.

Bi Onkwani atatoa uamuzi ikiwa atamwachilia kwa dhamana Bw Khan Jumatatu wiki ijayo.

Pia Bw Miller aliahidi kuwapeleka kwa DCI waliokuwa wakurugenzi wa benki hiyo Mabw  Duncan Kabui Gichu, James Mwaura Mwenja na Makarios Omondi Agumbi kuchukuliwa alama za vidole ndipo washtakiwe.

Washukiwa ambao hawakufikishwa kortini waliamriwa wafike mahakamani Septemba 17 kusomewa mashtaka dhidi yao.

  • Tags

You can share this post!

Mtu na mkewe kizimbani kwa wizi wa shamba la mamilioni

Man United itang’aa bila Pogba – Gary Neville

adminleo