Habari Mseto

'Kinara wa Chase Bank aliwapa watu wa familia mikopo ya Sh1b bila dhamana'

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA mwenyekiti wa benki iliyofilisika ya Chase Bank Mohammed Zafrullah Khan alitoa mikopo ya jumla ya Sh1 bilioni bila dhamana kwa kampuni za watu wa familia yake.

Bw Khan alimpa nduguye Mohammed Najifrullah  na mkewe Amira Claudia Wagner Khan mikopo ya Sh120 milioni bila kuweka dhamana kupitia kwa kampuni zao Golden Azure na Cleopatra Holdings Ltd.

Kampuni ya Goldeb Azure inayomilikiwa na Amira na Najifrullah ilipokea kitita cha Sh58,800,000 nayo Cleopatra ikatunukiwa Sh63.5 milioni.

Akifichua hayo , mfanyakazi wa Benki ya SBM ya Mauritius, iliyonunua benki hiyo iliyofilisika, Bw James Kinuthia Njoroge, alisema makampuni manne yanayohusishwa na Zafrullah , nduguye , Najifrullah , Amira na wafanyakazi wakuu wa benki hiyo ya Chase waliifilisi kwa kujipa mikopo ya zaidi ya Sh1.6bilioni.

Kampuni zilizopokea pesa bila kuweka dhamana na kupelekea benki hiyo kuanguka ni Cleopatra, Golden Azure, Colnbrook Holdings Ltd na Camellia Investments Limited.

Colnbrook na Camellia zilipokea zaidi ya Sh1 bilioni.

Zafrullah Khan (kulia) na waliokuwa wakuu wa benki ya Chase Bank Mabw Duncan Kabue Gichuhi, James Mwaura na Makarios Omondi Agumbi. Picha/ Richard Munguti

“Nilipokagua faili nne za makampuni haya niligudua zilipokea mikopo bila kuwasilisha dhamana kama inavyotakiwa kisheria,” alisema Njoroge.

Mahakama ilifahamishwa mikopo hii ilihidhinishwa na wakuu wa benki hiyo wanaoshtakiwa pamoja ndugu hao ilitolewa kinyume cha sheria.

Wakurugenzi hao hawakutoa anwani zao, hawakutoa taarifa ya kifedha ya makampuni hayo manne ,hawakutoa dhamana na kusimamia mikopo hiyo.

Wamekanusha mashtaka ya kufanya njama za kuilaghai benki hiyo, wizi na ulanguzi wa pesa.

Kiongozi wa mashtaka Bi Rubby Okoth alimweleza hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku kuwa kuna mashahidi 23 walioorodheshwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo ya kashfa ya Sh1.6bilioni.

Wengine walioshtakiwa ni pamoja waliokuwa wafanyakazi wakuu wa Chase Bank Mabw Duncan Kabue Gichuhi, James Mwaura na Makarios Omondi Agumbi

Kesi itaendelea Juni 12.