Kindiki asema ‘hapa kazi tu’ akikataa kuingizwa kwa siasa za Mlimani
NA WANDERI KAMAU
WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki, amewaonya wanasiasa dhidi ya kumwingiza kwenye siasa za urithi katika ukanda wa Mlima Kenya 2027.
Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakimtaja Prof Kindiki kuwa miongoni mwa viongozi ambao huenda wakachukua uongozi wa kisiasa katika eneo hilo kutoka kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Hata hivyo, Prof Kindiki alisema Jumanne kwamba “ninajishughulisha na kazi yake ya Uwaziri, kwani ina majukumu mengi”.
“Mijadala yoyote ya kisiasa kuhusu 2027 au uchaguzi mwingine wowote ule mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu haifai, na ni ya kijinga. Ni kama kuipaka tope demokrasia yetu. Rais Ruto amenipa jukumu la kuendeleza mipango ya utawala wake, ili kulifanya taifa hili kuwa mahali salama kwa vizazi vijavyo. Jukumu hili muhimu linahitaji kujitolea kwingi. Hivyo, lazima mtu ajitenge na mambo ambayo huenda yakaathiri utendakazi wake. Mjadala huo unafaa kukoma mara moja. Ikiwa utaendelea, naomba jina langu lisiingizwe ndani,” akasema Prof Kindiki kwenye taarifa.
Baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakitajwa kuwa na uwezekano wa kurithi uongozi wa ukanda huo ni mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, aliyekuwa kiongozi wa kundi la Mungiki Maina Njenga kati ya wengine wengi.
Prof Kindiki amekuwa akipigiwa upatu kuchukua uongozi wa eneo la Mlima Kenya Mashariki, linalojumuisha kaunti za Embu, Meru na Tharaka Nithi.
Viongozi wengine ambao wamehusishwa na kuchukua uongozi wa eneo hilo ni Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya na Gavana Cecily Mbarire (Embu).
Prof Kindiki alikuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa wakipigiwa upatu kuteuliwa na Rais Ruto kama mgombea-mwenza wake, kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.