Habari MsetoSiasa

Kingi awatetea MRC kuhusu haki za ardhi

June 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES LWANGA

GAVANA wa Kilifi, Bw Amason Kingi ametetea itikadi za kundi la Mombasa Repulican Council (MRC) akisema kuwa shinikizo za kundi hilo tata zinaangazia uhuru wa Wapwani kumiliki ardhi.

Kulingana na gavana huyo, haki za jamii za Pwani kumiliki ardhi zimekuwa zikikandamizwa tangu Kenya ipate uhuru miaka 56 iliyopita.

Bw Kingi ambaye alihadithia historia ya jinsi eneo la Pwani ambalo lilikuwa chini ya uongozi wa Sultani wa Zanzibar kabla ya kuunganishwa na sehemu nyingine za Kenya mnamo Oktoba 8, 1963 baada ya uhuru, alisema Waingereza waliokuwa wakitawala Kenya wakati huo hawakuzingatia jinsi Wapwani wangemiliki ardhi kutoka kwa Waarabu.

“Kundi la MRC limeelekea hadi mahakamani kupeleka malamishi yao kuhusiana na dhuluma za umiliki wa ardhi ambazo zinafaa kuangaziwa kwa kina,” alisema na kuongeza, “Kuwapiga na hata kuwaua haitaleta suluhisho.”

MALALAMISHI

Gavana alisema kwa vile serikali imekosa kusuluhisha malamishi ya MRC ambayo yanahusu Wapwani wote na kuacha masuala hayo kufanyiwa siasa, kundi hilo halitaangamizwa.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba haistahili kundi hilo kutumia vita kueneza misimamo yao.

“MRC si mtu bali ni itikadi. Yale ambayo sitakubali kama gavana ni uvamizi na mauaji ya watu wasio na hatia kisha wavamizi kujificha msituni, kwa sababu watu hao hawakuchangia kwa dhuluma,” akasema.

Serikali ilikuwa imepiga marufuku kundi la MRC hadi mnamo Julai 2016 wakati Mahakama ya Rufaa ilipitisha uamuzi sawa na mahakama kuu ya kuhalalisha kundi hilo.

“Dhuluma hizi zikikosa kutatuliwa, serikali hitaweza kuangamiza kundi la MRC na litaendelea kukaa kati yetu na ndiyo sababu makundi mengine ambayo yana maono sawia na MRC yatatokelezea kama vile Mulungu Nipe, Kaya Bombo na zenginezo,” akasema alipohutubu katika sherehe za Madaraka mjini Kilifi.

Bw Kingi alikuwa anaongea kuhusiana na madai kutoka kwa mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya, mbunge Michael Kingi (Magarini) na Seneta Stewart Madzayo kuwa polisi walikuwa wanawashika wakazi ambao wanapatikana wamevalia mavazi ya utamaduni wa Mijikenda wakiwasingizia kuwa wanachama wa MRC.

“Mavazi hayafai kutumiwa kutambua ni ni nani ni MRC, wakazi kuvalia mavazi meupe na mekundu ni kulingana na mila na tamaduni zetu na haifai kutumiwa kama sababu ya kusingizia mtu kuwa MRC,” alisema na akawaambia maafisa wa polisi wafanye uchunguzi wa kina baadala ya kuangalia mavazi.

Zaidi ya hayo, Bw Kingi alisema ardhi za Wapwani zilianza kutumika kama zawadi na viongozi serikalini kuwapa jamaa na marafiki zao.

Wiki iliyopita, kamati ya ardhi bungeni iliambiwa jinsi viongozi mashuhuri wakiwemo mawaziri, wabunge na wakuu wa serikali katika serikali ya KANU walijigawia ekari 470 kila mmoja katika shamba ya ADC eneo la Sabaki.