• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Kinoti atikisa korti tena, atia pingu hakimu

Kinoti atikisa korti tena, atia pingu hakimu

Na MOHAMED AHMED na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) ametikisa tena Idara ya Mahakama kwa kumkamata Hakimu Mwandamizi wa Mombasa Edgar Kagoni kwa madai ya kutoweka kwa dawa za kulevya za thamani ya Sh30 milioni.

Kukamatwa kwa hakimu huyo Ijumaa kulijiri wiki mbili baada ya Jaji Mkuu David Maraga kusema hatalinda afisa yeyote wa mahakama kukiwa na ushahidi kwamba alihusika na ufisadi.

Bw Maraga alisema hayo Agosti 23, 2019, wakazi wa Mombasa walipoandamana hadi mkutano wa majaji wakilalamika kuwa wanawasaidia walanguzi wa dawa za kulevya kuepuka adhabu.

Waandamanaji waliokuwa wamebeba mabango waliwashutumu majaji na mahakimu kwa kuendeleza ufisadi kwa kuwaachilia huru walanguzi wa mihadarati.

Jaji Maraga na majaji wote wa Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu walikuwa wanakongamana Mombasa wakati huo.

“Kazi yenu ni kupokea hongo na kuwaachilia walanguzi wa dawa za kulevya,” walilalamika mbele ya majaji.

Walikashifu idara ya mahakama kwa kushindwa kuwafunga walanguzi wa dawa za kulevya wa familia ya Akasha waliosukumiwa kifungo cha miaka 25 nchini Amerika

Wapelelezi walimtia nguvuni Bw Kagoni kwa tuhuma za kuhusika na kutoweka kwa dawa za kulevya za thamani ya Sh30milioni kutoka mahakama ya Mombasa.

Dawa hizo zilikuwa zimehifadhiwa kama ushahidi katika kesi ya ulanguzi wa mihadarati.

Mbali na dawa hizo baadhi ya maafisa wa mahakama hiyo ya Mombasa wanahojiwa kwa wizi wa Sh600,000 zilizonaswa na polisi wakisaka mihadarati.

Bw Kagoni alikamatwa pamoja na naibu wa afisa mkuu wa Mahakama ya Ruiru Bw Onesmus Momanyi, Bw Abdallah Awadh aliye naibu wa afisa mkuu wa mahakama ya Mombasa na Bw Lawrence Thoya, anayefanya kazi korti ya Mombasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya DCI, dawa na pesa hizo zilipotea Julai 2018. Hakimu huyo anazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Mombasa Port. Washukiwa hao watafikishwa kortini kesho kujibu mashtaka.

Kughushi

Kushikwa kwa Kagoni, kulitokea baada ya kukamatwa kwa karani wake Bi Florence Dianga kwa madai ya kughushi hati za kumwachilia kwa dhamana mfanyabiashara wa Mombasa Bw Mohammed Ali Noor.

Bi Dianga alishikwa pamoja na Bw George Ochieng Omollo na Teddy Ojwang Mwanga. Watatu hawa walishtakiwa katika mahakama ya Shanzu.

Kushikwa kwa Bw Kagoni kumefungua ukurasa mpya katika vita dhidi ya ufisadi na dawa za kulevya. Mwaka jana, mkurugenzi wa upelelezi wa jinai George Kinoti alimkamata Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kwa madai ya kutumia vibaya mamlaka yake.

Jaji Mwilu alipambana kortini na majaji watano wakatupilia mbali kesi dhidi yake. Hata hivyo, Mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP alikata rufaa na kuwasilisha ombi katika Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) akiomba Jaji Mwilu afutwe kwa madai ya ufisadi.

You can share this post!

Orengo akosoa Rais kuhusu mswada wa fedha

NiE: Base Titanium kufadhili shule 21 magazeti ya Taifa Leo

adminleo