Kinyozi asimulia anavyokabiliana na hali ngumu ya uchumi
Na SAMMY WAWERU
Jackson Muia amekuwa kwenye biashara ya kinyozi kwa zaidi ya miaka mitano. Ni mwendo wa saa sita za mchana na Taifa Leo Dijitali inampata anakofanyia kazi, eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.
Inachukua muda wa saa moja tukipiga gumzo bila kuona mteja yeyote, Jackson akieleza hiyo ndiyo imekuwa ratiba ya kila siku, kinyume na hapo awali kabla kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Covid – 19 kuripotiwa nchini. “Kidogo tunachopata tunashukuru Mungu,” Jackson anaeleza, akiongeza kusema kwamba mapato ya sasa ni ya mahitaji ya kimsingi pekee.
Mhudumu mwenza alienda mashambani, na kabla kurejea Rais Uhuru Kenyatta akawa ametoa amri ya kuingia na kutotoka kaunti ya Nairobi na viunga vyake. Amri hiyo pia imeshirikisha kaunti kadhaa eneo la Pwani. “Licha ya kuwa hayupo, idadi ya wateja ninaopata kunyoa ni ya chini mno,” Jackson anaendelea kueleza.
Dakika kadhaa baadaye, akiwa katika harakati za kusimulia biashara ya kinyozi ilivyoathirika kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona nchini, wateja wawili wanaingia. Anawahudumia kwa muda wa takriban dakika 40 kila mmoja.
Muda huo ni taswira ya hali ilivyo si tu katika kinyozi hicho, ila katika vinyozi na biashara zingine.
Kilio cha mfanyabiashara huyo kinawiana na cha Mzee Mark Mathenge, kinyozi eneo la Zimmerman, Nairobi. Mathenge ana vinyozi viwili na wakati wa mahojiano kwa njia ya kipekee aliiambia Taifa Leo Dijitali kwamba changamoto ni zile zile moja anazoshuhudia.
“Idadi ya wateja imeshuka kwa kiwango kikuu,” akalalamika. Licha ya kushusha bei, kutoka Sh70 – 50 ili kuvutia wateja, alisema juhudi hizo hazijazaa matunda yoyote yale.
Huduma za kinyozi na ususi, zimetajwa kama baadhi ya zilizo katika hatari kuchangia kuenea kwa virusi vya corona, vinavyosababisha ugonjwa wa Covid – 19. Hilo hasa linatokana na mtagusano kati ya mhudumu na mteja, wizara ya afya ikishauri wananchi kusitisha kupata huduma hizo kwa muda.
Aidha, umbali baina ya mtu na mwenzake ikiwa ni pamoja na kuepuka mkusanyiko wa watu, ni miongoni taratibu na sheria umma inahimizwa kutilia mkazo ili kuzuia maambukizi ya corona.
Wakati wa mahojiano, Jackson Muia alisema kwa sasa anapata kati ya wateja 10 – 15 kwa siku, na siku zingine wanakuwa chini ya 10. “Kabla ya janga la Covid – 19, kwa siku kila mmoja alikuwa akihudumia zaidi ya wateja 20, wikendi wanafikia 30,” akasema. Ada ya huduma zake ni kati ya Sh50 – 100.
Isitoshe, alilalamikia kupanda kwa bei ya jeli na sabuni, anazotumia kuosha na kupaka kichwa na kidevu cha mteja. Kwa mfano, dettol na spirit, alisema zimepanda mara dufu. “Zimepanda kwa zaidi ya asilimia 100, kuangushia mteja gharama hiyo ni kumfukuza,” alisema.
Jackson amezingatia utaratibu na sheria zinazotakikana, ambapo mteja sharti anawe mikono kabla kuingia, kupitia mtungi na jeli iliyoko mlangoni. Pia anavalia maski. Ameandaa kiti, kinachokaliwa na wateja wawili pekee, wakitakiwa kuzingatia umbali wa mita moja na nusu kati yao.
Licha ya biashara yake kudorora, Jackson ana imani, “imani kuwa Kenya na dunia itashinda vita dhidi ya virusi vya corona”. Kwa kuwa ni mcha Mungu, anaendelea kuiombea serikali katika jitihada zake kuangazia janga hili ambalo limehangaisha uchumi na Wakenya, ujumbe wake kwa wananchi ukiwa “tufuate taratibu na maagizo tunayopewa”.