Kioja wake kubadilishana waume
Na GAITANO PESSA
WANAWAKE wawili katika Kaunti ya Busia wameacha wakazi wa vijiji vya Siroba na Namuchula katika maeneobunge ya Matayos na Butula mtawalia, kwenye mshangao, baada ya kubadilishana wake wao.
Wake hao, Lilian Weta, 28, ambaye ni mama wa watoto watatu, na Millicent Auma, 29, mama wa watoto wawili walisema wameamua kubadilishana waume kufuatia mzozo ambao umekuwa ukikumba ndoa zao.
Bi Weta alifichua kuwa aliamua kutafuta mpango wa kando baada ya mumewe Kevin Barasa kuoa mwanamke mwingine mwezi mmoja uliopita.
Baada ya mumewe kumwoa Bi Auma, Weta aliamua kulipiza kisasi kwa kuanza uhusiano wa kimapenzi na mume wa zamani wa mke-mwenza, Christopher Abwire.
Baadaye Bi Weta aliolewa na Bw Abwire na kurasmisha ndoa yao wiki tatu zilizopita.
“Mume wangu (Barasa) mwezi mmoja uliopita alikuja na mwanamke nyumbani na akaniambia kwamba alikuwa binamu yake. Aliniagiza nimpikie chakula na baadaye nilimpeleka katika chumba cha kula,” Bi Weta akaambia ‘Taifa Leo’ katika makazi yake mapya.
Baada ya kumhoji zaidi, mgeni huyo aliyekuwa amevalia jaketi ya mumewe, alitishia kumshambulia kwa kisu na kutangaza kuwa mji huo ulikuwa wake.
“Aliniambia kwamba mume wangu alimtuma aniambie kwamba nilikuwa huru kuondoka na kuolewa kwingine,” akaelezea Bi Weta.
“Nilipiga simu nyumbani kwetu na jamaa zangu wakanishauri niondoke,” akaongezea.
Kwa upande mwingine, mumewe Bw Abwire alikuwa akimtafuta Bi Auma aliyeondoka bila kumfahamisha kabla ya kuambiwa kuwa tayari ameolewa na mume mwingine (Barasa).
Ni katika wakati huo ambapo Bi Weta alimtembelea Bw Abwire na kumfahamisha kuwa ndoa yake pia ilikuwa imesambaratika.
Bw Abwire alishawishi Bi Weta aishi naye na hata akamshauri alete watoto wake waishi pamoja.
Bw Abwire aliambia Taifa Leo kuwa amefurahia na kuridhishwa na uhusiano wake mpya.
“Tangu huyo mwanamke (Bi Auma) kuja hapa naishi kwa amani. Sisumbuki kama hapo zamani. Ananipa kila kitu ninachotaka,” akasema Bw Abwire.
Kwa upande mwingine, Bw Barasa alisema kuwa amefurahishwa na mke wake mpya.
“Sitajaribu kufuatilia mke wangu wa zamani kwani alikuwa mzigo kwangu,” akasema.
Wanakijiji wakiongozwa na Bw Hector Osuru walielezea mshangao wao kutokana na kitendo cha wanne hao.
“Sijawaji kushuhudia kitu kama hicho maishani mwangu. Kwa kuwa wao ni watu wazima wenye akili timamu tunaheshimu uamuzi wao alimradi wasizue vituko baadaye. Hayo ni maisha yao,” akasema Bw Osuru.