Shamba la Delmonte kukaguliwa upya na wizara
Na LAWRENCE ONGARO
WIZARA ya Ardhi ina mpango wa kukagua upya kipande cha ardhi cha Delmonte ili kuamua hatima ya shamba hilo.
Waziri wa Ardhi Faridah Karoney amesema wakati Wizara ya Afya itatoa ripoti yake kamili kuhusu ugonjwa wa Covid-19 kwamba mambo kurejea kawaida, ukaguzi wa ardhi hiyo utang’oa nanga.
Shamba hilo litapimwa upya ili kutambua mipaka halali baina ya mmiliki na upande wa umma ili igawanywe inavyostahili.
Bi Karoney ilikuwa akijibu hoja ya mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina iliyowasilishwa bungeni hivi majuzi kuhusu ardhi hiyo ya Delmonte ili iendeleze shughuli zake kwa kuongeza muda wa miaka 99 ili kuokoa hatima ya wafanyakazi zaidi ya 6,500 wanaofanya kazi huko.
Kampuni ya Delmonte imekuwa ikiendesha shughuli za kutengeneza juisi kutoka kwa mananasi kwa zaidi ya miaka 50.
Kulingana na nambari ya ardhi hiyo 12203 /1 na 12203/2 umiliki wake ulistahili kukamilika mwaka wa 2019.
Halafu kipande kingine cha LR No 1218 umiliki wake unastahili kukamilika mwaka wa 2022.
Mbunge wa Thika Bw Wainaina hivi majuzi alitetea shamba hilo ili kuokoa ujira na ajira ya wafanyakazi zaidi ya 6,500.
Alisema yeye kama mbunge wa Thika, ambako kampuni hiyo ipo, ni jukumu lake kutetea wafanyakazi hao wanaotegemewa na familia zao.
” Ni muhimu kutetea wafanyakazi hao kwa sababu wengi wanatoka Thika na vitongoji vyake na sio vyema kupoteza ajira wakati kama huu mgumu,” alisema Bw Wainaina.
Kwenye taarifa iliyowasilishwa na Bi Karoney, alisema wizara yake inafanya mazungumzo ya karibu na tume ya kitaifa ya ardhi (NLC), ili kufanya kikao maalum na kaunti mbili; Kiambu na Murang’a, ambazo ziko katika maeneo ya shamba kubwa la Delmonte.
Hata hivyo kuongeza muda mwingine wa kampuni ya Delmonte kuendelea na biashara zake kumepingwa na washika dau wengi wakidai shamba hilo liregeshewe serikali mara moja.