Habari Mseto

Kipchoge ajikuta kwenye zogo la mali linalohusisha wanandoa wawili

May 15th, 2024 3 min read

TITUS OMINDE NA LABAAN SHABAAN

WANARIADHA wawili mashuhuri wanahusika katika mzozo wa umiliki wa mali ya familia ya thamani ya Sh100 milioni.

Mvutano huu unahusisha aliyekuwa mwanariadha Daniel Komen na mke wake Joyce Kimosop Komen ambaye ni mhadhiri mkuu wa Chuo Kikuu cha Moi.

Bi Komen, amemshtaki mumewe, pamoja na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya Dunia ya Marathon na bingwa wa Olimpiki mara mbili Eliud Kipchoge.

Mwingine aliyehusishwa ni Brimin Kipruto, mshindi wa mbio za mita 3,000 za wanaume katika mbio za kuruka viunzi na maji kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing ya 2008.

Bi Komen amemshutumu mumewe kwa kuuza mali yao kwa washtakiwa wanne bila kumhusisha akisema ana hisa sawa katika ardhi hiyo.

Jaji Reuben Nyakundi wa Mahakama Kuu ya Eldoret ndiye mwamuzi wa kesi ya ardhi ya ekari 200 (L.R No. 8638/26.) iliyoko Kusini Mashariki mwa Manispaa ya Eldoret, Uasin Gishu.

Mke alishtuka kujua shamba limeuzwa

Bi Komen anasema alishtuka kugundua kwamba wanariadha Eliud Kipchoge, Brimin Kipruto na watu wengine wawili walidai mali hiyo ni yao.

Katika hatikiapo iliyowasilishwa kortini kupitia wakili wake Patrick Kibii, Bi Komen amewataja pia wakulima wa nafaka waliogeuka kuwa wanabiashara – Mabw Felix Kipchoge Lagat, na Peter Kipsigei Lagat.

“Pia nimeshangaa kwamba mali hiyo iliuzwa kwa Sh10 milioni tu, ambayo inawakilisha asilimia 10 tu ya thamani ya ardhi,” alisema katika nyaraka za mahakama.

Kulingana na Bi Komen, alichangia kiasi kikubwa cha pesa kustawisha mali hiyo, na kwa sasa ina thamani ya zaidi ya Sh100 milioni.

 “Mume wangu hajawahi kunitajia kwamba alikuwa ameuza shamba hilo,” aliteta Bi Komen anayepambana ili kulirudisha kwa familia.

Aliambia mahakama kwamba wote walistawisha mali hiyo, lakini ilisajiliwa kwa jina la mumewe kwa dhamana ya familia.

“Nilichukua mikopo ili kufadhili ununuzi na ujenzi wa makazi hayo – ilikuwa nyumba pekee ya familia kwani niliolewa na Komen wakati ambao hakuwa na mahali pa kuita nyumbani,” alisema katika nyaraka za mahakama.

Walifunga ndoa mnamo Novemba 5, 1998 na wamebarikiwa na watoto watatu.

“Nilizungumza na chifu wa eneo Bw Tarus, ambaye alipaswa kutoa kibali chake kama inavyohitajika, lakini aliniarifu hakuwa na taarifa ya mauzo,” akasema mke wa mwanariadha huyo.

Matakwa 5 ya Bi Komen

Ameorodhesha masuala matano ya kikatiba ambayo anataka Jaji aamue. Mojawapo ni kama mke wa Daniel Komen, ana haki ya kuhusika katika shughuli inayohusisha mali ya familia.

Bi Komen kadhalika anaomba mahakama ibaini kama kisa hiki kimekiuka haki zake za kikatiba.

Mahakama pia inatarajiwa kuamua ikiwa uuzaji wa ardhi hiyo umekiuka vipengee vya sheria.

Vile vile Bi Komen anaitaka mahakama itoe uamuzi kama ana haki (kama mke) ya kupata mgao sawa wa mali husika.

Pia anataka korti imfahamishe kama ana haki ya kupokea malipo yoyote ya fidia kutokana na kesi hii.

Komen ataka kesi iamuliwe faraghani

Komen amepuuzilia mbali madai ya mkewe aliyesema wanamiliki mali hiyo pamoja akieleza kuwa yeye ndiye mmiliki pekee aliyesajiliwa.

Hata hivyo, anakiri kuwa mlalamishi ni mke wake na wamejaliwa watoto.

“Ni kweli tuliomba mkopo wa Sh6 milioni pamoja ili kulipa salio lililobaki la bei ya ununuzi wa ardhi,” alikiri Bw Komen akiomba aruhusiwe kesi iamulie nje ya korti.

Pia anakiri kuwa aliuza mali ya ndoa kwa washtakiwa wanne, akiwemo Eliud Kipchoge, akidai ilikuwa kwa idhini ya mkewe.

Wanunuzi wajitetea

Katika hati yao ya kiapo kumjibu mlalamishi, washtakiwa wakiongozwa na Bw Eliud Kipchoge walisema kuwa Septemba na Oktoba 2011, waliarifiwa na Daniel Komen kuwa alikuwa na kipande cha ardhi ambacho alikusudia kukiuza.

“Tulimjulisha kuwa tulikuwa na nia ya kununua mali hiyo na ndipo Komen akatuuzia kwa  Sh10 milioni. Tulichunguza na kuthibitisha kwamba ardhi hiyo ilisajiliwa kwa jina lake,” alisema Bw Kipchoge.

Bw Kipchoge amesema wameweka walinzi na wafanyakazi watano ili kulinda mali hiyo inayozozaniwa.

“Mimi ni mnunuzi wa shamba hilo na sikujua kuhusu mzozo wowote,” alisema Bw Kipchoge.

Jaji Nyakundi amezitaka pande husika kufika mahakamani Jumatatu, Mei 20 kwa maelekezo zaidi.