Habari Mseto

Kitendawili ahadi ya Rais Ruto kuhusu hospitali ikipuuzwa

Na KEVIN CHERUIYOT September 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MNAMO Machi mwaka huu, Rais William Ruto alitembelea mradi uliokwama wa upanuzi wa Hospitali ya Mutuini Level 3 ulioanzishwa na Shirika la Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) lililovunjwa.

Serikali ya kaunti ya Nairobi ilieleza kuwa mradi huo ulihitaji Sh230 milioni ili ukamilishwe na hivyo kupandishwa hadhi kuwa hospitali kuu kutoka Level 3 hadi Level 5.

Kulingana na ajenda ya serikali ya kutekeleza mabadiliko katika sekta ya afya nchini, Rais alitangaza kuwa serikali ingewekeza fedha za kufanikisha kukamilishwa kwa mradi huo.

Aidha, Dkt Ruto aliamuru mwanakandarasi arejee kazini.

“Baada ya wiki mbili zijazo, nitatuma mwanakandarasi aje kukamilisha kazi hii ili miezi minne baadaye, turejee kuizindua. Nitarejea Agosti kuzindua mradi huu,” Rais Ruto akasema alipozuru hospitali hiyo akiandamana na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Hata hivyo, miezi mitano baadaye, mwanakandarasi hajakamilisha kazi. Hii ina maana kuwa Rais Ruto alikosa kuzindua mradi huo Agosti alivyoahidi mnamo Machi mwaka huu.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Mutuini, Dkt Martin Afred Wekesa, kukamilishwa kwa mradi huo kumechelewa kwa sababu ya kubadilishwa kwa muundo wa jengo la hospitali hiyo.

Dkt Wekesa ambaye alitumwa katika hospitali hii miezi mitatu iliyopita, anasema alilazimika kuangalia upya muundo wa hospitali na mahitaji muhimu yaliyokosekana.

“Tulifanya mabadiliko mengi ya ndani. Tulibadilisha orofa ya nne ili kutoa nafasi ya vyumba vya wadi ya wanaume na wanawake. Tulilazimika kubadilisha muundo wa vyumba vya upasuaji, tukaunda vyumba zaidi vya kuwahudumia wagonjwa wa figo,” akaeleza.

Dkt Wekesa alisema, awali, majengo ya hospitali hiyo yangejumuisha hifadhi ya maiti, wazo ambalo yeye alipinga.

Sababu nyingi ya kucheleweshwa kwa mradi huo ni kuagizwa kutoka ng’ambo kwa vifaa vya kujenga lifti, mfumo wa kutoa majitaka na vifaa vya kuunganisha umeme.

Uagizaji vifaa unafanywa na serikali ya kaunti kwa ushirikiano na Serikali Kuu.

Hata hivyo, Dkt Wekesa aliwahakikishia wakazi kuwa mwanakandarasi atakamilisha kazi “haraka”.

“Wakati huu, wafanyakazi wanahudumu kwa zamu mara mbili kwa siku. Wakati huu tumemaliza asilimia 75 ya kazi. Mwanakandarasi ametuhakikishia kuwa atakamilisha kazi kufikia mwishoni mwa Oktoba,” akasema.

Dkt Wekesa alisema kazi hiyo inasimamiwa na maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), ilivyokuwa nyakati za NMS.