Habari Mseto

Kitendawili cha vitabu 900 vya vyeti vya kuzaliwa vilivyoibwa katika afisi iliyo na ulinzi wa saa 24

Na KITAVI MUTUA October 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

AFISI ya usajili wa Raia, eneo la Mutomo, Kaunti ya Kitui, imepoteza tarakilishi mbili zenye data muhimu za usajili pamoja na vitabu 900 vya vyeti vya kuzaliwa baada ya wezi kuvamia afisi za serikali ikiwemo afisi ya Naibu Kamishna wa kaunti hiyo iliyo na ulinzi wa polisi saa 24.

Kulingana na Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Mutomo  Patrick Kafulo, uvamizi huo ulifanyika usiku wa Septemba 12 na kugunduliwa na wafanyakazi walioripoti kazini asubuhi iliyofuata.

Bw Kafulo alisema watu kadhaa wakiwemo wafanyakazi wa usafi na Msajili anayesimamia watu Bw James Khobes wameandikisha taarifa, lakini hakuna aliyekamatwa hadi sasa.

“Suala hilo bado linachunguzwa. Ingawa serikali imefuta vitabu hivyo. Tunataka kubaini nia ya wizi huo na kurejesha vifaa vilivyoibwa,” alisema Bw Kafulo.

Jumanne, Kaimu Katibu wa Huduma za Usajili wa Raia, Bw Paul Mwangemi, kupitia tangazo kwa umma, alionya kuwa vyeti hivyo katika kurasa 100 kila kitabu vilifutwa na kuwa ni batili.