• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Kituo cha kunyonyeshea watoto chazinduliwa

Kituo cha kunyonyeshea watoto chazinduliwa

Na WINNIE ATIENO

KITUO cha umma kwa wanawake kunyonyesha watoto wao, kimezinduliwa mjini Mombasa, ili kuwapa afueni mamia ya akina mama ambao huwa hawapati muda kwa kwenda nyumbani kunyoyesha wanapokuwa kazini.

Waziri wa afya katika kaunti hiyo, Bi Hazel Koitaba, alisema hatua hiyo itaimarisha afya ya watoto.

Takwimu za afya zinaonyesha asilimia 70 ya akina mama wananyonyesha mfululizo kwa kipindi cha miezi sita katika Kaunti ya Mombasa.

Kituo hicho kilifunguliwa katika makao makuu ya Huduma Centre, Mombasa na kitawasaidia akina mama wengi ambao wamekuwa wakitatizika wanapotaka kunyonyesha wanapotembea mjini wakisaka huduma za serikali.

“Hiki kituo kitasaidia wafanyikazi wa Huduma Centre na akina mama wanaotafuta huduma zetu. Mwanamke yeyote ambaye anataka kunyonyesha mtoto wake akiwa Mombasa anakaribishwa,” alisema afisa mkuu wa kituo hicho, Bw Alex Mureithi.

Kulingana na Bw Mureithi kituo hicho ndicho cha kwanza katika afisi za serikali nchini na kina maafisa wa afya watatu, jokofu la kuweka maziwa katika chupa ili yasiharibike, maji, sabuni na meza ya kumsafisha mtoto na kumbadilishia nguo au nepi.

Mkurugenzi wa afya katika kaunti ya Mombasa, Dkt Shem Patta, alisema kufunguliwa kwa kituo hicho ni hatua kubwa na kitawezesha wanawake kuwanyonyesha watoto wao kwa miezi sita kama wanavyopendekeza wataalam wa afya.

Serikali ya kaunti ya kituo cha Huduma kimeshirikiana kuhakikisha kina mama wananyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miezi sita bila kuwapa watoto wachanga uji au maji au chakula chochote ambacho si maziwa ya mama.

Wazazi na wakazi wa kaunti ya Mombasa walisifu hatua hiyo wakisema itawasaidia kunyonyesha watoto wachanga.

Wafanyikazi wa kituo hicho pia wamesema ni afueni kwao kwani wataendeleza shughli ya kunyonyesha watoto wao kwa kukama maziwa na kuweka kwa friji.

Kituo hicho kitakuwa kinasafishwa katika usafiw a hali ya juu ili kupunguza mamabukizi ya maradhi.

Afisa mkuu wa afya Dkt Aisha Abubakar alisema serikali ya kaunti itaendelea kuhamasisha kina mama kuendeleza zoezi la kunyonyesha watoto hadi miezi sita.

Serikali ya kaunti imesihi viwanda vya kibinafsi kuunda sehemu za kina mama ambapo wanaweza kunyoyesha au kukama maziwa kwa watoto wao.

“Tunapanga kuunda sehemu za kunyoyesha watoto ili kina mama wanaokuja kazini humu mjini waweze kunyoyesha watoto wao bila bugdha,” alisema Dkt Abubakar.

You can share this post!

Musila aanika ‘ujanja’ wa Kibaki dhidi ya Raila...

Wakenya wanataka kuhamia majuu kusaka ajira – Ripoti

adminleo