Habari Mseto

Kizaazaa malori ya muguka yakiingia Mombasa

May 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KEVIN MUTAI Na SIAGO CECE

KULIKUWA na mshikemshike katika eneo la Bonje jijini Mombasa wakati askari wa kaunti walijaribu kuwazuia wafanyabiashara wa muguka kuingia jijini humo.

Wafanyabiashara hao wa muguka, ambao walikuwa hawawezi kuingiza bidhaa hiyo Mombasa tangu Gavana Abdulswamad Nassir kutoa agizo kuu la kupiga marufuku matawi hayo mnamo Mei 22, 2024, walifika Bonje mnamo Jumatano asubuhi na malori yao yakisafirisha bidhaa hiyo.

Walichukua hatua hiyo baada ya mahakama ya Embu kutoa maagizo ya kuzuia kwa muda maagizo makuu ya magavana wa Mombasa, Kilifi na Taita Taveta kutekeleza marufuku ya muguka.

Askari wa kaunti walisisitiza kwamba walikuwa wakisubiri kupokezwa stakanadhi za agizo hilo lililotolewa na Jaji Lucy Njuguna mnamo Jumanne kwenye kwenye kesi iliyowasilishwa na chama cha muguka cha Kutherema na Serikali ya Kaunti ya Embu. Kesi hiyo dhidi ya marufuku hayo itasikilizwa mnamo Juni 8, 2024.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wa muguka walikasirishwa na kukaa kidete kwa askari hao, wakidai walikuwa wanachelewesha bidhaa hiyo inayoharibika haraka.

Baadhi ya askari na wauzaji muguka walipigana hali iliyofanya askari wa kaunti kuondoa magari yao waliokuwa wametumia kufunga barabara.

Askari mmoja wa kaunti alionekana na nguo zilizokuwa zimeraruka kutokana na vuta nikuvute hiyo ya dakika chache.

Baada ya sokomoko hiyo, wauzaji wa muguka walingurumisha malori na yakaingia kubwaga muguka kwa soko kubwa la Kongowea, tayari kusambaziwa wateja wengi waliokuwa wakisubiri.

Soma Pia: Search muguka Maswali mengi kuhusu ‘ulezi’ uliotumbukiza Wapwani kwa uraibu wa muguka

Mapema wiki hii, ilifichuka kwamba Kaunti ya Kwale ambako masharti yalikuwa yamelegezwa, ilikuwa ikitumika kama kitovu cha magendo kuingiza muguka katika kaunti jirani ya Mombasa.

Uchunguzi wa Taifa Leo uligundua magari ya muguka yalikuwa yakiingia hadi Kinango kutokea makutano ya Samburu-Kinango katika barabara kuu ya Nairobi-Mombasa.

Madereva wa magari hayo walikuwa wakipita Kinango, Kwale mjini na kisha katika makutano ya Kombani, ambayo ni barabara inayounganisha kaunti za Kwale na Mombasa.

Hapo Kombani, muguka ulikuwa ukiwekwa kwa vifurushi vipya na kisha kuingizwa kisiri Mombasa kupitia kivuko cha Likoni.

Gavana wa Kwale Fatuma Achani aliwahakikishia wakazi hangepiga marufuku muguka, lakini angetumia sheria na masharti magumu.

Akihutubia wanahabari katika afisi yake, Bi Achani alisema kuwa serikali yake ilikuwa imeweka hatua madhubuti ikiwemo ushuru wa juu zaidi katika mwaka ujao wa kifedha ili kupunguza athari mbaya za muguka kwa wakazi.

Mswada wa Fedha wa Kaunti ya Kwale wa 2024 ambao sasa uko katika Bunge la Kaunti, ulipelekwa kwa umma ambapo wenyeji na wakazi walitoa maoni yao kuhusu matumizi ya muguka katika eneo hilo.

Kulingana na Mswada huo, wakazi walitaka kuongezwa kwa ada ya kiingilio cha magari ya muguka kutoka Sh10,000 hadi Sh100,000 kwa kila gari linaloingia katika kaunti hiyo, wakibaini kuwa hiyo ndio njia bora zaidi ya kudhibiti biashara ya muguka.

Wafanyibiashara wa Muguka katika Kaunti ya Kwale hata hivyo walipinga hatua hiyo ya kuongezwa kwa ada, wakisema itaathiri biashara zao.

“Tuna furaha kwamba Gavana amezingatia kwamba biashara husaidia watu wengi katika kaunti hii. Tunajua biashara hiyo inafanywa na wenyeji wa hii kaunti na wale wa kutoka bara. Wengi wetu tumekuwa tukitegemea biashara hii kuendeleza maisha yetu. Itakuwa si haki ikiwa leseni na mapato yataongezwa na hivyo kufanya iwe vigumu kwetu kumudu,” alisema Bi Pauline Kathure, mwakilishi wa wafanyabiashara hao.

Bi Philomena Mutua, ambaye anauza chingamu za kutafuna, alisema anategemea biashara ya muguka ambayo huchochea ‘wachongaji’ kununua chingamu.

“Biashara ya muguka ikifeli, inamaanisha kuwa biashara yangu pia itafeli na sitaweza kukidhi mahitaji ya familia yangu,” alisema Bi Mutua.

Muguka katika Kaunti ya Kwale huuzwa katika pakiti za Sh50 na kuifanya bidhaa hiyo iwe rahisi kwa watu wengi.