Kizimbani kwa kuiba mamilioni ya Airtel
Na BENSON MATHEKA
WAFANYAKAZI wawili wa kampuni ya mawasiliano ya Airtel, wameshtakiwa kwa kuiba zaidi ya Sh244 milioni kutoka kwa kampuni hiyo.
Bw Wellingtone Kibendi Momanyi 35, ambaye alikuwa ameajiriwa kama karani wa pesa na Eric Mutua Wambua 27 aliyekuwa nyapara, Jumanne walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Barbara Ojoo kujibu shtaka la kuiba mali ya mwajiri wao.
Walikanusha kwamba kati ya Desemba 29 2015 na April 19 2018 katika ofisi za kampuni ya Airtel Kenya zilizoko barabara ya Mombasa walishirikiana na watu wengine ambao hawakuwa kortini kuiba Sh244,694,903 mali ya kampuni hiyo.
“Siku tofauti kati ya Desemba 29 2015 na Aprili 19 mwaka huu katika kampuni Airtel Kenya, Nairobi, mlishirikiana na watu wengin e kuiba pesa hizo,” shtaka lilieleza.
Shtaka lilisema kwamba walipata pesa hizo wakiwa wafanyakazi wa kampuni hiyo. Kulingana na ripoti ya uchunguzi wa kesi, ilidaiwa kwamba walikuwa wakilenga baadhi ya maajenti na wateja wa kampuni hiyo.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba kampuni ilifichua wizi wa pesa hizo baada ya kufanya uchunguzi wa kina. Kwenye taarifa zao kwa polisi, washtakiwa wanakiri kwamba walikuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo na kueleza majukumu waliyokuwa wakitekeleza.
Hata hivyo wanakanusha madai ya wizi wa pesa za mwajiri wao. Kila mmoja aliachiliwa kwa dhamana ya Sh10 milioni na mdhamini wa kiasi sawa au walipe Sh1 milioni pesa taslimu kupata uhuru wao.
Kesi hiyo itatajwa Mei 8 ili washtakiwa wakabidhiwe taarifa za mashahidi na itaanza kusikilizwa Juni 27 mwaka huu.