• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kizimbani kwa kutumia jina la Ruto kuiba vipakatilishi 2,800

Kizimbani kwa kutumia jina la Ruto kuiba vipakatilishi 2,800

Na Richard Munguti

MWANAMUME aliyetumia jina la Naibu wa Rais William Ruto kupokea vipakatilishi 2,800 zenye thamani ya Sh180 milioni alishtakiwa Jumatatu katika Mahakama ya Milimani, Nairobi.

Bw Daddy Awiti alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Bw Awiti alikabiliwa na mashtaka mawili kuwa kati ya Juni 16 na Agosti 12 mwaka huu jijini Nairobi alifanya njama za kulaghai alitengenezea cheti cha zabuni iliyokuwa na jina la Naibu wa Rais William Ruto akidai alikuwa amekubaliwa kuwasilisha tarakilishi 2,800 zenye thamani ya Sh180 milioni.

Kiongozi wa mashtaka Bi Kajuju Kirimi alisema mshtakiwa alijifanya alikuwa amepewa jukumu la kupeleka tarakilishi hizo kwa afisi ya Bw Ruto.

Bi Kirimi alisema mshtakiwa alipokea tarakilishi hizo 2,800 muundo wa HP Laptops kutoka kwa kampuni ya Makindu Motors Limited iliyoko barabara kuu ya Mombasa-Nairobi kwa njia ya undanganyifu.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema mshtakiwa alipokea tarakilishi hizo akishirikiana na watu wengine akijua alikuwa anadanganya, afisi ya naibu wa rais haikuwa ikihitaji tarakilishi hizo.

“Ni kweli ulipokea tarakilishi hizo ukitumia jina la Naibu wa Rais Bw Ruto?” Bi Mutuku alimuuliza.

“Sio kweli. Sikuchukua tarakilishi hizo,” Bw Awiti alijibu.

Mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana.

“Unapinga ombi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana,” hakimu alimuuliza Bi Kirimi.

Akijibu, kiongozi wa mashtaka alisema hapingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana ila aliomba korti itilie maanani kiwango cha pesa ambacho kilikuwa kinahusika.

Bi Mutuku alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa anayefikishwa mahakaman hata kama anakabiliwa na shtaka lipi.

Hata hivyo, alisema mahakama inaweza kumnyima mshtakiwa dhamana ikiwa upande wa mashtaka utawasilisha ushahidi kuonyesha kuwa “atavuruga mashahidi ama kuhitililafiana na utekelezaji wa haki.”

Korti ilisema upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi unaothibitisha kuwa mshtakiwa hatafika mahakamani wakati wa kusikizwa kwa kesi inayomkabili.

“Hii mahakama imetilia maanani ushahidi uliowasilishwa na mshtakiwa kwamba atafika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi inayomkabili,” alisema hakimu.

Alimwagiza mshtakiwa alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh3 milioni kabla ya kuachiliwa kutoka rumande.

Mahakama iliteua Septemba 10 2018 kuwa siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo.

Pia hakimu aliamuru kesi hiyo itajwe kesho (Agosti 22) kuunganishwa na kesi nyingine ambapo washukiwa walikuwa wameshtakiwa hapo awali.

Pia mahakama iliamuru Bi Kirimi amkabidhi mshtakiwa nakala zote za mashahidi aandae utetezi wake.

  • Tags

You can share this post!

Mama asukumwa jela miaka 8 kwa kukata nyeti za mumewe

ONYANGO: Mjadala wa kuhalalisha bangi haufai kupuuzwa

adminleo