Habari Mseto

Kizimbani kwa kuuma polisi sikio kisha kumzaba kofi

December 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MBURURAJI mkokoteni alishtakiwa Jumanne kwa kumuuma afisa wa trafiki wa sikio na kumzaba konde mdomoni na kumsababishia majeraha.

Peter Kirimi Kanogi almaarufu Tosi alifunguliwa mashtaka mawili na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) ya kumjeruhi afisa wa kulinda usalama.

Katika shtaka la kwanza mshtakiwa alikabiliwa na shtaka la kumjeruhi afisa wa Polisi na kukataa kutiwa nguvuni.

Katika harakati za kutiwa nguvuni mshtakiwa alizua vurugu , ndipo akamuuma sikio afisa huyo wa polisi sikio na kumwacha majeraha.

Hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot, alielezwa na kiongozi wa mashtaka Bw Bernard Panyako kuwa afisa huyo wa Polisi Mutuku Kitavi anayehudumu katika kituo cha Polisi cha Central alikuwa na wenzake wakishika doria katika makutano ya barabara ya Accra na Tsavo Nairobi.

“Konst Kitavi alipokea habari kutoka kwa umma kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa na kisu na alikuwa anamwandama mwenzake amtoe uhai,” hakimu alifahamishwa.

Bw Panyako alisema Konst Kitavi na mwenzake walimkimbiza mshtakiwa na kumzingira.

Mlalamishi alimshika mshtakiwa na kumpkonya kisu alichokuwa akitaka kukitumia amdunge mwenzake waliyekuwa wamezozana.

“Alipoona amenyang’anywa kisu, mshtakiwa alimrukia afisa huyo wa polisi akamshika na kumuuma sikio la upande wa kulia,” Bw Panyako alidokeza.

Mahakama ilifahamishwa hasira za mshtakiwa zilikuwa bado kutulia na alimchapa masumbwi mazito afisa huyo wa polisi na kumpasua mdomo.

“Ni ukweli ulifanya hayo?” hakimu alimwuliza mshtakiwa. “Sikujua ikiwa mwanamume niliyemkabili alikuwa afisa wa polisi,” akajibu Kanogi.

“Hii mahakama imechukulia umekanusha shtaka,” hakimu alimweleza mshtakiwa. Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana.

“Sipingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana ila naomba mahakama itilie maanani mshtakiwa alimshambulia na kumwumiza afisa wa kudumisha usalama,” Bw Panyako aliambia korti.

Mahakama ilimwachilia Kanogi kwa dhamana ya Sh600,000.

Kesi itatajwa Desemba 24 kutengewa siku ya kusikizwa.