Kizimbani kwa kuiba Sh213 milioni za kaunti
Na RICHARD MUNGUTI
WAFANYAKAZI saba wa zamani wa kaunti ya Nairobi waliokuwa wamejificha Jumatatu walishtakiwa kwa ulaghai uliopelekea gatuzi hili kupoteza zaidi ya Sh213 milioni.
Hakimu mwandamizi mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Lawrence Mugambi alifahamishwa kuwa mamilioni haya yalilipwa kampuni mbili Ngurumani Traters Limited (NTL) na Lodward Wholesalers Limited (LWL) kati ya 2014 na 2016.
Saba hao walifikishwa kortini baada ya kujisalimisha kwa maafisa wa tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC jana asubuhi.
Ijumaa iliyopita hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti alitoa kibali cha kuwatia nguvuni washukiwa hao baadaya kuelezwa walikosa kufoka kortini Agosti 9 kushtakiwa pamoja na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero aliyeshtakiwa pamoja na afisa mkuu wa fedha Bw Maurice Okere.
Bw Ogoti alitoa kibali washikwe na kufikishwa kortini kujibu mashtaka ya ubadhirifu wa mali ya umma.
“Licha ya kibali kutolewa cha kuwashika, ni Bw Jimmy Mutuku Kiamba aliyekuwa mhasibu mkuu alifika mbele ya tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC Jumapili,” kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Njeru alimweleza Bw Mugambi huku akiomba wanyimwe dhamana na wazuiliwe gerezani.
“Washukiwa hawa hawawezi kuaminika.Hatuna uhakika ikiwa wakiachiliwa watafika kortini,” alisema Bw Njeru, akiongeza , “Walipewa fursa wajinusuru tabia yao lakini wakajisaliti. Wanyimwe dhamana.”
Mawakili Cliff Ombeta na James Ochieng Oduol wanaowatetea washtakiwa waliomba mahakama iwaachilie kwa dhamana kama iliyopewa Dkt Kidero ya Sh2milioni pesa tasilimu kisha wawasilishe mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.”
Walioshtakiwa mbele ya Bw Mugambi ni Lilian Wanjiru Ndegwa, Jimmy Mutuku KIamba , Geoffrey Mwangongo, Stephen Ogago Osiro, Luke Mugo Gatimu, John Githua Njogu, Grace Njeri Githua , Lodwar Wholesalers Limited (LWL) na Ngurumani Traders Limited (NTL).
Washtakiwa hawa walikanusha shtaka la kupelekea serikali kupoteza zaidi ya Sh213milioni kwa kulipa makampuni ya Nguruman na Lodwar kwa huduma ambazo hazikutolewa.
Washtakiwa hao walikabiliwa na mashtaka 34.
Mahakama iliombwa itaje kesi hiyo Septemba 7 pamoja na kesi ya Dkt Kidero na Bw Okere kwa maagizo zaidi.
Bw Mugambi aliwaachilie kwa dhamana sawa na Dkt Kidero na kuagizwa wawasilishe vyeti vyao vya kusafiri kortini.
Washtakiwa walikabiliwa na mashtaka mbali mbali kulingana na majukumu waliyotekeleza walipokuwa wameajiriwa na kaunti ya Nairobi chini ya himaya ya Dkt Kidero.