KMPDU yamlaumu Kagwe kwa kudai madaktari wanapata corona wakiwa nje ya hospitali
Na SAMMY WAWERU
MASLAHI ya madaktari na wahudumu wa afya kipindi hiki hatari cha janga la Covid-19 lazima yaangaziwe.
Muungano wa Madaktari Wataalamu wa Dawa na Madaktari wa Meno (KMPDU) pia umesema lazima wahudumu wa afya walindwe dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona, wakati wakiwa kazini.
Akieleza kughadhabishwa kwake na matamshi ya hivi punde ya Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe kuwa ‘wahudumu wa afya na madaktari wanaambukizwa corona nje ya kazi’, Kaimu Katibu Mkuu wa KMPDU, Dkt Chibanzi Mwachonda alisema viongozi wa miungano inayotetea haki za wahudumu hao hawataruhusu madaktari kuangamia kwa kile ametaja ni chocheo la utepetevu wa serikali.
Kwenye kikao na wanahabari mnamo Jumanne, jijini Nairobi, Dkt Mwachonda pia alitoa ilani ya mgomo kuanza baada ya wiki mbili ikiwa matakwa ya wahudumu wa afya hayataangaziwa.
“Hatutakubali madaktari wetu na wahudumu wa afya kuangamizwa na corona. Hii kauli ya Waziri kuwa madaktari wanaambukizwa corona wakiwa nje ya hospitali sharti ikome,” akasema.
Dkt Mwachonda pia alieleza kushangazwa kwake na matamshi “madaktari na wahudumu wa afya wanapata corona wakiwa kwenye baa”, ambapo aliyataja kama “cheche za matusi kwa wahudumu wanaojitolea kuhatarisha maisha yao kulinda Wakenya dhidi ya Covid-19”.
Katibu huyo alisema mahangaiko ya wahudumu wa afya yanatokana na suala la viongozi serikalini, hasa waliotwikwa jukumu katika idara ya afya, kueneza mahusiano mema kwa umma, ilhali mambo nyanjani ni tofauti na tetesi zao.
Aidha, alisisitizia haja ya tume ya afya kubuniwa ili kusaidia kutatua mahangaiko ya wahudumu wa afya nchini.
Mwezi huu wa Novemba 2020 taifa limepoteza idadi kubwa ya madaktari na wahudumu wa afya, walioangamizwa na makali ya virusi vya corona.
Madaktari wanalalamikia upungufu na ukosefu wa vifaa kujikinga kuambukizwa corona (PPE), kati ya vinginevyo.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini, juma lililopita, Waziri Kagwe hata hivyo alisisitiza kwamba kuna vifaa vingi na vya kutosha vikiwemo PPE katika ghala la Mamlaka ya Usambazaji Dawa na Vifaa vya Kimatibabu (KEMSA).