Kongamano kuandaliwa kuzima utovu wa usalama
Na PETER MBURU
WAKAZI wanaoishi maeneo kame yanayopambana na ukosefu wa usalama wana kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali kutangaza kuandaa kongamano litakalojadili matatizo hayo na suluhu zinazohitajika Septemba.
Kongamano hilo litaandaliwa kupitia idara ya serikali ya maendeleo ya maeneo kame (ASAL), wizara ya ugatuzi Malindi, kaunti ya Kilifi kati ya Septemba 5 na 7 na litajumuisha kaunti 29 zilizoorodheshwa kuwa kame.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa maeneo hayo, ambayo mengi yako kaunti za kaskazini mwa taifa kukongamana kwa nia ya kujadili matatizo yanayowakumba kwa nia ya kupata suluhu.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi Jumatatu, waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa na Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal walisema kuandaliwa kwake kutatumika kama njia ya kuainisha mipango ya maendeleo ya kaunti zilizoko katika maeneo kame na malengo ya taifa ya siku za usoni.
“Washirika watakua na fursa ya kuoanisha malengo ya maendeleo ya kaunti zilizoko maeneo kame na ruwaza ya taifa ya 2030, malengo ya maendeleo ya mkondo wa tatu (MTP III), malengo ya maendeleo ya dunia (SDGs) na ajenda nne kuu za serikali (Big 4 Agenda),” akasema Bw Wamalwa.
Baadhi ya masuala yanayotarajiwa kupewa kipau mbele wakati wa kongamano hilo ni uchumi, mazingira, uongozi na masuala ya kitamaduni, ambayo yametajwa kuwa ufunguo wa wa maendeleo ya sehemu hizo.
“Kwenye masuala ya uchumi, suala la utoshelezaji wa chakula, kuinua kilimo cha mifugo, ujenzi na uinuaji na ujenzi wa viwanda vitajadiliwa. Aidha namna ya kupunguza makali ya ukame na adhari za mabadiliko ya anga ni masuala yatakayopewa umuhimu,” akasema Bw Lenolkulal.
Masuala ya amani katika maeneo ambayo fujo na mizozo vimekuwa ada ya siku, afya na lishe bora na elimu, masuala ya jinsia na utunzaji wa wazee na watu wenye ulemavu aidha yameorodheshwa kujadiliwa.
Kongamano hilo litaandaliwa kwa ushirikiano kati ya serikali kuu, serikali za kaunti na mashirika ya kibinafsi.