Korti kuamua Agosti 8 ikiwa Waititu ataendelea na kazi
Na RICHARD MUNGUTI
GAVANA wa Kiambu Ferdinand Waititu Jumatatu alijitetea vikali katika Mahakama Kuu akitaka kuruhusiwa kutekeleza majukumu ya ugavana kesi inayomkabili ya ufisadi wa Sh51.2 milioni ikiendelea kusikizwa.
Jaji Ngenye Macharia ataamua ombi hilo la Bw Waititu Agosti 8, 2019.
Kupitia kwa mawakili Prof Tom Ojienda na Nelson Havi, Bw Waititu alimsihi Jaji Ngenya Macharia abatilishe uamuzi ulioagiza asitekeleze majukumu ya ugavana hadi kesi aliyoshtakiwa katika kashfa ya Sh51.2milioni isikizwe na kuamuliwa.
Prof Ojienda aliomba Bw Waititu akubaliwe kurejelea majukumu yake ya ugavana akisema agizo la hakimu mkuu Lawrence Mugambi kumzima asiende kazini “ ni kumwachisha kazi.”
“Hakuna agizo la mahakama linaweza kumtimua Gavana yeyote kazini. Bw Mugambi alitafsiri vibaya uamuzi wa Jaji Mumbi Ngugi alitoa akisema Gavana akishtakiwa asiendelee na kazi hadi kesi aliyoshtakiwa isikizwe na kuamuliwa,” Prof Ojienda alisema Wakati huo huo, Prof Ojienda pia alisema kwa sasa mahakama inakabiliwa na hali ya sintofahamu kwa vile imeacha kufuata sheria na utaratibu wa tangu jadi kwamba mshukiwa apewe dhamana kulingana na kiwango anachodaiwa aliiba ama kupora.
Wakili huyo alimsihi Jaji Macharia asimame imara na kutetea ugatuzi kwa kubadili masharti ya dhamana aliyopewa Gavana Waititu.
Aliomba mahakama kuu ipunguze kiwango cha dhamana cha Sh15milioni pesa taslimu hadi Sh1milioni ama Sh2milioni kwa vile anakabiliwa na shtaka la upokeaji wa Sh51.2milioni.
Kuwahusu Waziri wa Ujenzi katika kaunti ya Kiambu Bw Luka Mwangi Waihinya almaarufu Lucas na mmiliki wa kampuni ya Testimony iliyopewa kandarasi ya kujenga barabara katika kaunti hiyo, Prof Ojienda aliomba dhamana yao ya Sh15 milioni pesa taslimu zipunguzwe hadi Sh5milioni kwa vile wanakabiliwa na ufisadi wa Sh588milioni.
Wakili huyo alimweleza jaji huyo kuwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Henry Rotich aliachiliwa kwa dhamana sawa na Bw Waititu ilhali anadaiwa kuhusika na ufujaji wa zaidi ya Sh63bilioni katika kashfa ya mabwawa ya Kamwerer na Aror.
Prof Ojienda alisema Vifungu 181, 182 na Sheria za kupambana na ufisadi (Aceca) 66(2) vimeeleza wazi wazi jinsi ya kumtoa gavana kazini.
Lakini viongozi wa mashtaka Alexander Muteti na Victor Owiti walipinga mawasilisho hayo na kusema Bw Mugambi hakukosea kamwe ila alitumia sheria jinsi ilivyo. Bw Muteti alisema mahakama zapasa kupambana ufisadi kwa nguvu ilizopewa na katiba na sheria za kukabiliana na ufisadi.
“Bw Waititu hapasi kuruhusiwa kurudi kazini hadi mahakama inayosikiza kesi inayomkabili na mkewe Susan Wangari isikizwe na kuamuliwa,” alisema Bw Muteti.