Habari Mseto

Korti yaagiza ukaguzi KTDA baada ya kilio cha wakulima

October 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na NDUNGU GACHANE

MAHAKAMA imeagiza ukaguzi kufanyiwa rekodi za fedha za Mamlaka ya Ustawishaji wa Majanichai (KTDA) kufuatia kushuka kwa mapato ya wakulima mwaka 2019.

JAJI Kanyi Kimondo wa Mahakama ya Murang’a aliagiza Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kukagua mapato ya majani chai, bonasi na mazao yaliyowasilishwa KTDA katika mwaka wa 2018 na 2019.

Hii ni baada ya Gavana wa Murang’a, Mwangi Wa Iria kuwasilisha ombi la kuwekwa wazi kwa umma akaunti za KTDA kutokana na kupungua kwa mapato ya majani chai.

Kwenye kesi kati ya serikali ya Kaunti ya Murang’a dhidi ya KTDA, utawala wa kaunti unataka akaunti hizo ziwekwe wazi kwa umma ikisema kuna tashwishi kuhusu ripoti ya ukaguzi wa hesabu iliyowasilishwa na mamlaka hiyo.

Pengo la Sh2.6 bilioni kwenye mapato ya mwaka wa 2018 na 2019, ambayo ni asilimia 36, ndiyo ndilo imechochea kaunti kutaka akaunti hizo zifanyiwe ukaguzi.

Kulingana na KTDA, mapato ya majani chai mnamo 2018 yalikuwa Sh11.2 bilioni huku yale ya 2019 yakiwa Sh8.9 bilioni.

Mapato hayo yamesababisha malalamiko kutoka kwa wakulima katika kaunti zinazokuza majani chai za Murang’a, Nyeri, Kiambu, Kirinyaga, Meru, Embu, Nandi, Kisii, Kericho, Bomet na Nyamira.

Lavutia hisia

Wakili Charles Njenga anayewaongoza mawakili sita kwa niaba ya wakulima, alieleza korti kwamba suala hilo limevutia hisia za umma na lisipoangaziwa kwa makini, wakulima watang’oa majani chai yao na hivyo kuathiri vibaya uchumi wa taifa.

“Hii ni shida kubwa na isipotatuliwa wakulima watang’oa majani chai na hilo litaathiri vibaya uchumi wa nchi,” akasema Bw Njenga.

Jaji Kimondo alitaja kesi hiyo kama ya dharura na kusema katiba inampa mkaguzi mkuu mamlaka ya kukagua akaunti zote kisha kuwasilisha ripoti ya shirika lolote linalofadhiliwa na fedha za umma.

“Nimeridhika kwamba suala hili ni la dharura na tukisubiri kusikizwa kwa kesi hii, namwagiza mkaguzi akague vitabu vya KTDA kisha kuwasilisha ripoti hapa mahakamani kabla ya Oktoba 28,” akaamuru.

Kwa upande wake, KTDA ilisema iko tayari kufanyiwa ukaguzi wa kifedha na kusisitiza kuwa shughuli za mamlaka hiyo zinafanyika kwa uwazi.