• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Korti yakubali ushahidi kuhusu shamba la Sh8 bilioni uliodaiwa kuwa feki

Korti yakubali ushahidi kuhusu shamba la Sh8 bilioni uliodaiwa kuwa feki

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Alhamisi ilikubalia ushahidi uliowasilishwa na mwanasheria mkuu kutoka kwa tume ya kupambana na ufisadi nchini (EACC) kuthibitisha nakala za umiliki wa shamba la ekari 134 lenye thamani ya Sh8 bilioni, uliodaiwa kuwa feki.

Jaji Elijah Ombaga alipokea ushahidi huo wa mwanasheria mkuu akisema atautegemea kuamua mmiliki halisi wa shamba hilo linalokumbwa na utata.

Ombi la kukataliwa kwa ushahidi huo liliwasilishwa na aliyekuwa meneja mkuu hazina ya malipo ya uzeeni NSSF Bw Josphert Konzollo anayetetewa katika kesi hiyo na wakili Steve Gikera.

Akiwasilisha ushahidi huo Bw Konzollo alisema mahakama haiwezi kuukubali kwa vile ulichunguzwa wakati EACC haikuwa na makamishna.

Makamishna wa EACC wakiongozwa na mwenyekiti wao Mumo Matemu walijiuzulu na kung’atuka mamlakani.

Bw Konzollo aliomba mahakama isikubali ushahidi uliowasilishwa na EACC kupitia kwa wakili wa Serikali Allan Kamau kwa niaba ya mwanasheria mkuu (AG).

Lakini ombi hilo la Bw Konzollo lilipingwa vikali na mawakili Cecil Miller , Bw Kamau na Peter Wena anayewakilisha makamu wa zamani wa rais Bw Moody Awori.

Mzozo wa umiliki wa shamba hilo unang’ang’aniwa na kampuni ya Muchanga Investments Limited (MIL) ya marehemu Horatius Da Gama Rose na Bw Awori.

Akitoa uamuzi Jaji Ombaga alisema ushahidi unaopingwa ulinakiliwa kabla ya Bw Matemu na wenzake kujiuzulu.

“Ushahidi unaopingwa na Bw Konzollo kupitia kwa kampuni yake Telesource Limited ulinakiliwa kabla ya kujiuzulu kwa Bw Matemu. Unakubalika na hii mahakama itautegemea kama ushahidi,” alisema Jaji Ombaga.

Punde tu alipoutoa ushahidi huo Bw Gikera aliomba kesi hiyo isitishwe kusikizwa awasilishe rufaa.

Lakini Bw Miller alipinga akisema kesi hiyo imekaa kortini kwa muda wa miaka mitano na kamwe haipasi kusitishwa.

Bw Kamau aliomba mahakama iamuru Bw Gikera awasilishe ombi rasmi ndipo waijibu.

Jaji Ombaga alikataa kuisitisha akisema imekaa kortini kwa siku nyingi lakini akamruhusu Bw Gikera kukata rufaa.

Mfanyabiashara Catherine Njeri Ng’ang’a na Josphert Konzollo (kati). Picha/ Richard Munguti

Na wakati huo huo Jaji Ombaga aliamuru afisa mkuu aliyechunguza umiliki wa kesi hiyo afike kortini kutoa ushahidi kuhusu mmiliki halisi.

Jaji huyo alifahamishwa na wakili mwingine William Arusei anayemtetea Bi Catherine Njeri aliyeteuliwa na Jaji Aggrey Muchelule kumwakilisha marehemu Cermelina Ngami Mburu anayedai kuwa mmiliki wa shamba hilo kwamba atawasilisha ombi , mashahidi waliotoa ushahidi akiwamo mwanawe Da Gama Rose , Bw Dimitris na Bw Konzollo warudi tena kortini awahoji.

Marehemu Carmelina alikuwa ameolewa na aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Nairobi marehemu John Mburu.

Jaji Muchelule alimruhusu Catherine kutetea haki za Carmelina katika kesi hiyo.

Jaji Ombaga aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 21, 2019.

Na wakati huo huo akamwagiza Inspekta Mkuu Patrick Maloba kufika kortini kutoa ushahidi.

Wengine watakaotoa ushahidi ni pamoja na msajili wa ardhi Wanderi Muigai . wakili wa benki ya Barclays na mkurugenzi wa usorovea Pauline Gatimu. Mashahidi hawa watatoa ushahidi kuhusu mmiliki halisi wa shamba hilo.

MIL imeeleza korti ilinunua shamba hilo kutoka kwa benki ya Barclays kwa bei ya Sh1.2milioni naye Bw Konzollo anadai aliinunua kwa Bw John Kamau kwa bei ya Sh96milioni.

Umiliki wa shamba hili umezua malumbano makali hata Polisi wakatumwa mle shambani kuilinda isiingiliwe na yeyote.

Bw Miller anayewakilisha MIL amesema shamba hilo linamilikiwa na mteja wake ilhali Bw Konzollo anadai ni lake.

  • Tags

You can share this post!

Wakili kutoka Uingereza aruhusiwa kuongoza mashtaka dhidi...

KAHUHO TITANS: Timu iliyostawishwa kwa utu Kabete

adminleo