• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:00 PM
Korti yapiga marufuku uchochezi na ushambuliaji wa wapenzi wa jinsia moja

Korti yapiga marufuku uchochezi na ushambuliaji wa wapenzi wa jinsia moja

NA PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA imepiga marufuku makundi ya watu wanaopinga ushoga na kueneza uchochezi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja nchini.

Mahakama Kuu imetoa agizo hilo la muda kwenye kesi ambapo walalamishi wameomba agizo la kuzuia wanaharakati wanaopinga ushoga, na Mbunge wa Nyali Mohamed Ali, kuwachochea wananchi kuwaua au kuwadhuru kivyovyote watu wanaojitambulisha kama wapenzi wa jinsia moja (LGBTQ).

Agizo la Jaji Olga Sewe pia linawazuia wanaharakati hao pamoja na mbunge huyo kushinikiza kufurushwa nje ya nchi kwa watu wanaojitambulisha kama LGBTQ au kufungwa kwa mashirika yanayohudumia jamii hiyo ya LGBTQ.

“Kwa sasa, agizo la muda linatolewa kulingana na maombi nambari tatu ya ombi ili kuweka hali ilivyo sasa kubakia vivyo hivyo kabla ya kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi,” alisema Jaji Sewe.

Shirika la kutetea haki za jamii za wachache la Centre for Minority Rights and Strategic Litigation (CMRSL) na Bw JM wanataka uamuzi wa mahakama utolewe ya kuwa watu wa LGBTQ wana haki ya kulindwa kwa msingi wa katiba licha ya mwelekeo wao wa jinsia.

CMRSL na Bw JM walitaka maagizo ya muda kutolewa kuwazuia mbuge wa Nyali Bw Mohamed Ali, Salim Said, Athman Ahmed na vuguvugu dhidi ya LGBTQ kutekeleza mauaji kinyume cha sheria au kudhuru watu wanaojihusisha na LGBTQ.

Shirika hilo na Bw JM pia wanataka agizo litolewe na mahakama ya kuwa Bw Said, Ahmed, vuguvugu la kupinga LGBTQ, na Bw Ali wameenda kinyume cha katiba kuhusiana na maandamano yao ya kupinga jamii ya LGBTQ.

CMRSL na JM wanadai ya kuwa Bw Said, Ahmed, Ali na vuguvugu hilo la kupinga LGBTQ lilifanya maandamano katika barabara za Mombasa na baadaye kufanya mkutano katika uwanja wa Makadara ambapo waliwaambia wananchi wawauwe mashoga na wasagaji kulingana na sheria za kidini.

Haki ya kulindwa

Wanadai kuwa washtakiwa hao wametishia kufunga mashirika yanayotoa huduma au kuangalia ustawi wa watu ambao wanajitambulisha kuwa wa jamii ya LGBTQ.

“Mshatakiwa wa tano (Bw Ali) akiwa anawahutubia waliokuwa wakifanya maandamano aliitisha kuwauwa na kufurushwa Kenya kwa watu wanaojitambulisha kama LGBTQ,” stakabadhi za kesi hiyo zinasema.

Kando na Bw Said, Ahmed, Ali na vuguvugu linalopinga LGBTQ kuwa washtakiwa, Inspekta Jenerali wa polisi ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo.

Shirika la kitaifa la kutetea haki za kibinadamu, Amnesty International-Kenya, Shirika la Kenya la Kutetea haki za binadamu na tume ya uwiano na maridhiano (NCIC) zimetajwa kama wahusika muhimu katika kesi.

Katika hati yake ya kiapo aliyokuwa ameiwasilisha mahakamani, mbunge wa Nyali Bw Ali alisema kuwa hajawahi kuwa muhusika wa kupanga maandamano dhidi ya mashoga na wasagaji.

Bw Ali aliongeza kusema kuwa amewahi kuhudhuria maandamano hayo kama mkenya yeyote anayetekeleza haki yake ya uhuru wa kujieleza.

Mbuge huyo wa Nyali alikanusha madai ya kuwa hutekeleza jukumu la kuwachochoea wananchi dhidi ya jamii ya LGBTQ. Kesi itasikizwa Juni 24.

  • Tags

You can share this post!

Maji kwa vipimo Thika mitambo ya kupampu ikisombwa na...

Sarah afichua sababu ya kukatalia mbali penzi la Diamond...

T L