Habari Mseto

Korti yavunja ndoa ya mwanariadha wa kimataifa na mume aliyemtelekeza

Na TITUS OMINDE October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA ya Eldoret imekubali mwanariadha mstaafu wa kimataifa kumtaliki mumewe wa miaka 15.

Mwanariadha huyo mstaafu SJC, mama wa watoto wanne, aliruhusiwa kumtaliki mumewe MB, ambaye pia ni mwanariadha wa zamani wa mbio za marathon, baada ya mahakama kupata ndoa yao haingeweza kurekebishwa licha ya juhudi kadhaa.

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa kortini, wanandoa hao walifunga ndoa rasmi mnamo Januari 30, 2008, chini ya Sheria ya Ndoa.

Mkimbiaji huyo maarufu wa mbio ndefu aliwasilisha kesi ya talaka mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Eldoret Peter Ireri akimshtumu mumewe kwa ukatili na uasherati wakati wa ndoa yao.

Mwanariadha huyo alidai kuwa mbali na kumnyima haki yake ya ndoa, MB amekuwa akimdhulumu mara kwa mara kimwili, kihisia, kisaikolojia na kumtusi akilewa.

Katika kesi yake, SJC aliambia mahakama kwamba mumewe alimuacha yeye na watoto wao kwenye nyumba yao ya ndoa, na majaribio kadhaa ya kuokoa ndoa yao yameambulia patupu.

“Ndoa yetu ya miaka 15 imevunjika kiasi cha kutorekebishwa na hakuna nafasi ya kufufuliwa ikizingatiwa kwamba sote tumeendelea na maisha yetu,” SJC aliambia mahakama kupitia hati yake ya kiapo.

Mumewe hakujibu kesi ya mkewe waliyeachana na badala yake aliachia mahakamani kutoa uamuzi wake.

Akitoa uamuzi wake, Hakimu Mwandamizi alibainisha kuwa hakukuwa na ubishi kwamba ndoa kati ya wanandoa hao ilikuwa imesambaratika.

“Nimeridhika kwamba SJC na MB wamethibitisha sababu za talaka zilizotolewa chini ya kifungu cha 65 cha sheria ya ndoa, hivyo ndoa yoyote iliyokuwepo kati yao imevunjika kiasi cha kutorekebishwa na itakuwa ni haki ndoa yao iliyofeli kuvunjwa,” ilisema Hakimu Mwandamizi Ireri.

Hakimu alieleza kuwa hakuona sababu ya kukataa ombi la SJC la kutalikiana na mumewe kwa sababu ndoa yao haiwezi kudumu tena.

“Mahakama hii haiwezi kuamuru wahusika waendelee kuwa katika ndoa na uhusiano uliofeli. Ni kwa sababu hii natangaza kwamba ndoa kati ya wanandoa hao imevunjika na hivyo imevunjwa,” aliamuru hakimu.

Visa vya unyanyasaji wa majumbani miongoni mwa wanariadha wa Kenya vinaendelea kudhihirika kwa njia tofauti, huku baadhi ya wanariadha wa kike walioathiriwa wakiomba talaka..

Mwezi mmoja uliopita, mwanariadha wa Uganda wa mbio za marathon Rebecca Cheptegei, 33, alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya mpenzi wake wa zamani kudaiwa kumwagilia petroli na kumchoma moto nyumbani kwake Endebess, Kaunti ya Trans Nzoia.

Miaka mitatu iliyopita, mwanariadha wa mbio ndefu Agnes Tirop aliuawa huko Iten katika kesi nyingine ya unyanyasaji wa nyumbani, na mumewe waliyeachana anayekabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama Kuu ya Eldoret.

Marehemu Tirop alidaiwa kuuawa kwa kudungwa kisu na mumewe Ibrahim Rotich ambaye hatimaye alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA