Korti yawaachilia wanakamari 13 wakasajiliwe Huduma Namba
Na RICHARD MUNGUTI
WACHEZA kamari 13 waliokiri kuendeleza uhalifu barabarani katika jiji la Nairobi walikuwa na bahati ya mtende walipoachiliwa wakasajiliwe kwa Huduma Namba.
Kumi na tatu hao waliotiwa nguvuni Ijumaa wakijaribu bahati yao “kujitajirisha kwa kuwakanganya wapita njia” walinyenyekea mbele ya Hakimu Mwandamizi Kennedy Cheruiyot na kuapa kutorudia uovu huo.
Washtakiwa hao walimweleza hakimu, “ Hii ndiyo mara yetu ya kwanza kukamatwa na kufikishwa kortini kwa kucheza kamari kinyume cha sheria za bahati nasibu.”
Akiungama makosa mbele ya mahakama, Benson Muciri Gaitho alisema: “Mimi nakiri nilinyakwa na polisi nikicheza kamari nje ya makavazi ya kitaifa-(Kenya National Archives). Nilikuwa na wanadada hawa- Laura Wambui, Zaituni Wanjiku, Veronica Njeri na Judy Karimi.”
Kabla ya kuendelea hakimu alimwuliza Muciri, “Je, uko na Huduma Namba?”
Muciri: Hapana sijajisajili.
Hakimu: Kwa nini?
Muciri: Nilipoteza kitambulisho changu lakini nimepata fomu ya kubadilisha
Hakimu: Ukipewa fursa utajisajili?
Muciri: Naam.
Kundi la pili la wacheza kamari liliwajumuisha washtakiwa wanane Robert Kamau Kago, Stephen Asenyo Avisi, Jane Nduku King’oo, Colline Wangari Thurura, Josphine Kalunde Nzive, Rose Akinyi Adera, Lucy Wanjiku Ndung’u na Juliah Wanjiru.
Washtakiwa hao wote 13 walimsihi hakimu awaachilie.
Lakini Robert Kamau Kago, alipoona, mambo huenda yakamwendea mrama, aliamua kusema ukweli na kufichua, “Mimi nilikuwa nimechomoka kwa duka la dawa kununua dawa.”
“Nilikuwa nimeenda kununua dawa hizi na barua ya hospitali ni hii,” Bw Kago alimweleza hakimu na kuongeza, “Nilipotoka tu nilikamatwa. Mimi sikuwa nikicheza kamari. Nilikuwa nahofia maisha yangu.”
Mshtakiwa alimkabidhi hakimu madawa na barua ambazo zilipitishwa kwa kiongozi wa mashtaka Bw Kennedy Panyako.
“Je, unasemaje kumuhusu Bw Kago?” hakimu akauliza.
“Naomba kesi inayomkabili itamatishwe chini ya kifungu 87(a) cha sheria za uhalifu,” akajibu.
Hakimu alimwachilia na kumwagiza aende kutumia dawa.
“Kwenye barua hiyo daktari amesema hautumii dawa ipasavyo. Kunywa dawa. Umesikia? Hii mahakama imeakuachilia,” Hakimu Cheruiyot akamwambia.
Akiwaachilia Bw Cheruiyot alisema : “Uchezaji kamari umekuwa changamoto na janga la kitaifa. Maelfu ya wacheza kamari wamejihusisha na uovu huu ambao umekuwa changamoto kwa serikali. Hawa ni wachache tu waliokamatwa ikitiliwa maanani maelfu na malefu ya vijana wamejiingiza katika uovu huu.”
Bw Cheruiyot aliwahurumia washtakiwa hao na kuwaachilia wakachukue Huduma Namba inayoendelea kuandikishwa.
“Mko na Huduma Namba?” Bw Cheruiyot aliwauliza washtakiwa.
Walimjibu kwa sauti moja , “Hapana. Hatujajisajili. Twaomba utupe muda tukajiandikishe.”
Akijitetea pamoja na wenzake Bw Benson Muciri Gaitho alimweleza hakimu kuwa “ni umaskini uliowasukuma kwa kukaidi sheria.”
“Mheshimiwa ukitusukuma jela hatutapata Huduma Namba. Kule gerezani maafisa wanaopeana nambari hii hawamo. Twakusihi kwa mapenzi yako utuhurumie tu. Tusamehe. Hatutarudia makosa haya,” mmoja wa washtakiwa hao Muciri alimsihi hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot.
Washtakiwa wote walifurahi na kuahidi “Hatutarudi tena kucheza kamari. Tutafuta njia mbadala ya kutafuta riziki.”
“Kuna kazi nyingi za kufanya,” alisema Hakimu Cheruiyot huku akiwashauri, “Nendeni kwa MCA wenu mumweleze awatafutie kazi kama alivyoahidi vijana siku za kampeni.”