• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Korti za Kenya ni nzuri ajabu, raia wa Burundi asema baada ya kusamehewa

Korti za Kenya ni nzuri ajabu, raia wa Burundi asema baada ya kusamehewa

Bw Rukinguka Innocent akiwa katika Mahakama ya Milimani, Nairobi Aprili 3, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA wa Burundi Jumanne aliinua Biblia Takatifu kortini na kukiri kuiba Sh51,000 kisha akaachiliwa baada ya kuomba msamaha.

“Nakiri mbele ya hii korti kwamba niliiba pesa hizo. Natubu mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya hii mahakama na kuapa kwamba sitarudi kuiba tena,” Bw Rukinguka Innocent alisema huku akiinua Biblia.

Bw Innocent alisamehewa na hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi alipomsihi “asimpeleke jela kwa vile ameteseka sana na ametoroka nchi alikozaliwa kwa sababu ya siasa.”

“Ikiwa unajua uliiba pesa hizi inua Bibilia na kumuomba Mungu msamaha na hii mahakama,” Bw Andayi alimtaka mshtakiwa.

Mshtakiwa ambaye hakimu alisema hapasi kuitwa Innocent (mtu asiye na makosa) aliiomba korti msamaha na pamoja na mlalamishi.

“Nilishawishika kuiba pesa hizo kutoka kwa mlalamishi niliyempa makao jijini Nairobi. Mlalamishi anatoka katika lile kabila linalotaabisha kabila letu huko nyumbani Burundi,” alisema Bw Innocent.

Mshtakiwa alisema hata jijini Nairobi mlalamishi alimtaabisha sana.

Bw Innocent alisababisha kicheko alipoambia korti , “Mlalamishi alinisumbua na kunitesa kwa minajili ya masuala ya kisiasa tukiwa nyumbani na hapa sasa anaendelea kuniandama.”

Korti iliondoa mashtaka dhidi ya Bw Innocent chini ya kifungu cha sheria za uhalifu nambari 204 sheria za Kenya.

Baada ya kusamehewa mshtakiwa aliondoka kizimbani mwingi wa shukrani kwa Bw Andayi na kuapa , “Sitarudi kuiba tena. Korti za Kenya ni nzuri ajabu sana.”

  • Tags

You can share this post!

Walimu waliotumwa kufundisha maeneo hatari walia kukosa...

Aliyejifanya Sabina Chege kuwatapeli wabunge kupimwa akili

adminleo