KRA kunadi magari 568 yaliyokwama bandarini
Na BERNARDINE MUTANU
Ikiwa uliagiza gari kutoka nje ya nchi na bado hujalichukua baada ya miezi kadhaa, huenda ukalipoteza.
Hii ni baada ya Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini (KRA) kutangaza kuwa itanadi magari 568 yanayomilikiwa na watu 100 kutokana na kuwa yamekaa sana bandarini.
Kulingana na mamlaka hiyo, itachukua hatua hiyo kwa lengo la kupunguza msongamano forodhani.
Katika tangazo katika gazeti rasmi, KRA imewapa wamiliki hao siku 30 kuchukua magari yao ikiwa wanataka kuepuka mnanda.
Magari hayo ni tofauti tofauti yakiwemo magari ya kifahari kama Mercedez Benz, Toyota Land Cruiser na Toyota Prado na yale ya gharama ya chini kama vile Toyota Probox.
Kati ya magari yanayokabiliwa na mnada ni gari la Jesus is Alive Ministries, lake Margaret Wanjiru.
Wanaotaka kununua magari hayo wamealikwa na meneja wa operesheni za bandarini wa KRA Joseph Kaguru kutazama magari hayo Desemba 17 na Desemba 18.