Habari Mseto

KRA na NBK kuwapa vijana mafunzo ya ushuru na uwekezaji

May 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

WATOAJI wa huduma wa Mamlaka ya Kutoza Ushuru nchini (KRA) waliojisajiliwa katika mradi wa serikali wa nafasi za uagizaji (AGPO) watanufaika baada ya KRA kuingia katika mkataba na Benki ya National (NBK).

Mkataba huo ulitiwa sahihi Jumatano, Mei 23, katika afisi kuu ya KRA, Nairobi na ulishirikisha Kamishna Mkuu wa KRA John Njiraini na Mkurugenzi Mkuu wa KRA Wilfred Musau.

Katika taarifa, KRA ilisema watoaji 903 wa bidhaa na huduma waliosajiliwa na KRA miongoni mwao vijana, wanawake na watu walio na ulemavu watanufaishwa na mkataba huo.

Kutokana na mkataba huo, wahusika watanufaika kutokana na upokeaji wa mafunzo kutoka KRA kuhusiana na uagizaji, utaratibu na sheria kuhusu ushuru.

NBK kwa upande mwingine itawasaidia watoaji hao kupata elimu kuhusu ujasiriamali.

Zaidi, NBK imezindua hazina ya kuwafadhili watoaji hao, hasa watakaopata tenda za utoaji huduma na bidhaa kwa KRA kutoka afisi za KRA kote nchini.

Akiongea wakati wa shughuli hiyo, Bw Musau alisema, “Ushirika huo ni ushahidi kwamba benki ya NBK inatimiza malengo yake ya kutoa nafasi kwa wananchi wote kupata ufadhili wa kifedha.”