• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 AM
Krismasi bila shangwe

Krismasi bila shangwe

Na SAMMY WAWERU

Kwa kawaida maadhimisho ya Krismasi nchini Kenya na mataifa mengine duniani kila mwaka husheheni mbwembwe na shangwe, ila ya mwaka huu wa 2020 yameonekana ‘kutulia’.

Usiku wa kuamkia Desemba 25, wengi hushiriki mkesha katika maeneo yao ya kuabudu. Hata hivyo, 2020 mambo ni tofauti kabisa kutokana na hali ilivyo, ambayo imechangiwa na kuwepo kwa janga la Covid-19.

Mikesha ya kuadhimisha kusaliwa kwa Yesu Kristu mwaka huu imepigwa marufuku, kutokana na kuendelea kutekelezwa kwa sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia msambao wa corona.

Ni janga ambalo limeathiri na kuyumbisha sekta nyingi zinazochangia kuboresha uchumi, kuanzia ile ya utalii, uchukuzi, afya…kati ya nyinginezo.

Huku wengi wa wanaoishi mijini wakipuuza himizo la Wizara ya Afya, “hakuna haja ya kusafiri mashambani kipindi hiki virusi vya corona vinatesa”, wahudumu wa matatu nao wametumia mwanya huo kuvuna hela kwa kupandisha nauli mara dufu.

Kwa kawaida, Sikukuu ya Krismasi madhehebu mbalimbali huandaa ibada ya misa, ambayo hufuatwa na sherehe za mlo.

Baadhi ya maeneo ya kuabudu Desemba 25, 2020 yamesalia kufungwa kutokana na sheria na mikakati iliyowekwa na Wizara ya Afya kuzuia msambao wa Covid-19. Picha/ SAMMY WAWERU.

Mwaka wa 2020, taswira hiyo haijashuhudiwa, maagizo ya kutekeleza misa chini ya saa chache yakiheshimiwa. Baadhi ya makanisa milango yake imesalia na kufuli, siku kutwa.

Miaka ya awali, msimu wa Krismasi barabara nyingi nchini watu huonekana wakielekea kujivinjari. Mwaka huu, hata zile za mashinani idadi ya watu wanaoonekana ni ya chini mno.

Athari zilizosababishwa na virusi vya corona ni bayana kwa wamiliki na wahudumu wa bucha, ambao huvuna pantosha msimu wa Krismasi.

“Msimu huu biashara ya nyama iko chini sana. Shamrashamra za Krismasi hunogesha uuzaji wa nyama, ila mwaka huu wateja ni wa kuhesabika,” John Gichia mmiliki wa bucha eneo la Zimmerman, Nairobi, ameambia Taifa Leo Dijitali.

Leah Gitahi, mzaliwa wa Nyeri japo anafanya kazi Naivasha anasikitikia maadhimisho ya mwaka huu, kwa kile anataja kama “uliojaa matatizo”.

“Ninahimiza watu watulie waliko badala ya kujilimbikizia mzigo wa gharama ikikumbukwa Januari 4, 2021, majuma mawili kuanzia sasa, wazazi watarejesha wanao shuleni,” Leah anashauri.

Mama huyo ambaye ni muuguzi anakiri Krimasi ya 2020 haina shangwe wala vifijo, kutokana na mhangaiko wanayopitia Wakenya.

  • Tags

You can share this post!

Hospitali ya Gatundu yapanda ngazi

Shoo ya #WifeMaterial yamtia Eric Omondi matatani