Kuna mafuta ya kutosha Lokichar, Tullow Oil yasema
Na BERNARDINE MUTANU
KAMPUNI ya mafuta ya Tullow Oli imeidhinisha kuwepo kwa mafuta ya kutosha eneo la Lokichar, yanayoiwezesha kuanza biashara ya kuuza bidhaa hiyo.
Katika taarifa, Tullow Jumatano ilisema visima 21 vimechimbwa Lokichar katika shughuli ya kutathminiwa.
Kulingana na kampuni hiyo, eneo la Lokichar Kusini lina takriban mapipa 4 bilioni ya mafuta.
Tullow pamoja na Venture Partners imeshauri serikali kwamba bloku za Amosing na Ngamia zinafaa kuwa za mwanzo katika uchimbaji wa mafuta hayo Lokichar Kusini.
Shughuli ya kuanza kuchimba mafuta inatarajiwa kuanza robo ya kwanza ya 2018, kulingana na taarifa hiyo, ambapo mafuta yatakayochimbwa yatahifadhiwa mpaka idhini itolewe na mikakati ikamilike ya kusafirisha mafuta kwa barabara hadi Mombasa.