• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Kundi la kina mama linavyotumia biashara ya miche kukomesha wizi wa mifugo  

Kundi la kina mama linavyotumia biashara ya miche kukomesha wizi wa mifugo  

NA OSCAR KAKAI

KWA miongo mingi, eneo la Sarmach kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Turkana limekuwa likigonga vichwa vya habari kwa mambo mabaya.

Makumi ya watu wameuawa, mamia kupoteza makao na mifugo kuibwa tangu mwishoni mwa mwaka huu suala ambalo limechangia kudorora kwa uchumi.

Isitoshe, maboma yamesalia mahame, mashamba yakiachwa na mazao kuharibika.

Eneo hilo kame lenye utata, halikaliki kutokana na mashambulio ya mara kwa mara.

Licha ya kuwa na kiangazi na mimea mikavu na misitu kwenye milima na mabonde na hali ya mauti, eneo hilo sasa lina kiti cha maana ambacho Wakenya wengine wanafaa kujifunza.

Kina mama wa mashinani wenye hadithi za ufanisi wamepiga teke maovu kwa kushiriki katika kilimo cha miche ya miti, hali ambayo inaashiria kuleta mabadiliko kwa maisha ya jamii ya wafugaji kama njia mojawapo kudumisha amani na kukomesha wizi wa mifugo.

Chini ya mwavuli wa kikundi cha Kalya (Amani), wanajituma kuangazia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miche wanayouza kujipa mapato.

Aidha, inajumuisha miti yenye thamani hasa ya matunda kama vile; maembe, parachichi, paipai na mwarobaini.

Mradi huo ulioanzishwa 2021, na tayari unaashiria kuzaa matunda hasa katika utunzi wa mazingira, kando na kina mama washirika kujiendeleza kimaisha.

Mwenyekiti wa kundi hilo, Martha Longra anasema kuwa mradi huo unasaidia kupunguza suala la kutegemea mifugo kujikimu maishani.

Anasema kuwa wao huuza miche ya maembe ya kupandikiza (grafted) kwa Sh120, kila moja, na mingine kuanzia Sh100.

“Sisi huuza miche kwa shirika la Safer World,” alisema.

Anaeleza licha ya hali ya utovu wa usalama, shirika hilo sasa linahusika na upanzi wa miti ili kuimarisha hali ya anga.

“Tumeona biashara yetu ikichangia mazingira kuboreka, na tunahimiza kina mama wengine kujiunga nasi,” alisema.

Kupitia jitihada za Kalya, wana imani milio ya risasi na ujahili itaisha.

Sarmach ni kati ya maeneo tata Bonde la Ufa yanayozidi kuhangaishwa na ujangili; wizi wa mifugo.

Bi Martha anasikitika kwamba wenyeji hulazimika kufunga biashara jua linapotua kwa sababu ya utovu wa nidhamu.

Anaeleza kuwa akina mama wamepata ujuzi na mafunzo na wamekuwa mabalozi kuboresha mazingira, hatua inayowawezesha kujizimbulia riziki.

“Mpango huu umebadlisha maisha yetu pakubwa. Sasa tunaweza kupeleka watoto wetu shuleni bila kuhangaika, na kuna amani katika maboma yetu,” anasema.

Kutokana na mafunzo ya shirika la Safer World, kikundi hicho kimeimarisha uzalishaji wa miche ya miti na kupata ujuzi.

Malengo ya kikundi hicho ni kuongeza idadi ya miti Pokot Magharibi.

Kando na biashara ya miche, kinainuana kwa kuchangiana fedha.

Mwanachama Asha Ekuman anasifia mpango huo kuimarisha uchumi wa eneo hilo.

“Licha ya changamoto za utovu wa nidhamu, tunaona uchumi wetu ukiimarika,” Asha anasema.

Mratibu wa Kenya Pastoralists Commmunity Organization(Kepaco), shirika la vijana kuhubiri amani, Diana Rotich anasema kuwa eneo hilo lina wajane na wazee wengi waliofiwa kutokana na ujahili na huwapa ushauri ili waweze kurejea makwao.

Kulingana na Diana, shirika hilo husaidia akina mama ambao wameumia kutokana na visa vya utovu wa usalama.

Victor Ijaika, afisa msimamizi Tume ya Uwiano na Maridhiano (NCIC) Kaskazini mwa Bonde la Ufa, anapigia upatu kundi la Kalya akisema limeonyesha kuna uwezekano wa mashambulizi ya mara kwa mara kukoma.

“Wanachohitaji wakazi ni biashara inayowaingia mapato ili waondokee maovu,” anasema afisa huyo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kilio cha msichana aliyepita KCPE 2023 kukosa kujiunga na...

Askofu Yohanna akiri ni mfuasi wa Arsenal na atazidi kutoa...

T L