Habari Mseto

Kundi la wenye magari kuwapa chakula wakazi wa pato la chini

June 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Klabu ya magari ya Bundu Rovers imeanzisha kampeni ya kuhamasisha wananchi kuhusu athari za mafuriko ya hivi majuzi, ikiwa ni pamoja na njaa.

Klabu hiyo ilizindua kundi la magari 25 aina ya land rover katika ziara ya kilomita 2000 inayofahamika kama ‘Desert Drive against Hunger’.

Kundi hilo njiani litagawa chakula na bidhaa zingine kwa jamii zinazohitaji. Akiongea wakati wa uzinduzi  huo Alhamisi, mwenyekiti wa Bundu Rovers Rikky Aguda alisema, “Ajenda yetu ni kuacha historia njema katika jamii ambazo tutapitia. Tutasaidia katika kuimarisha viwango vya chakula nchini.”

Mafuriko yalisababisha uharibifu mkubwa wa mimea katika baadhi ya maeneo hali inayotishia usalama wa chakula maeneo hayo.

“Tunajua hatuwezi kusaidia kila mtu, lakini tutasaidia washikadau wetu kama vile Misheni ya Katoliki North Horr. Tutatoa kidogo tulicho nacho kuzisaidia jamii,” aliongeza.

Safari hiyo inatarajiwa kuanza Jumamosi Juni 23, 2018 Nairobi na magari hayo yatapitia North Horr, Kaunti ya Marsabit, Chalbi Desert, Mbuga ya Wanyamapori ya Sibiloi, Loiyangalani, Laisamis, Nanyuki  na kurejea Nairobi Julai 1 baada ya siku tisa kichakani.