Habari Mseto

Kundi lawapa vijana mafunzo kama njia mojawapo ya kuzuia mimba za mapema

August 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na DIANA MUTHEU

KUNDI moja la vijana katika Kaunti ya Mombasa limeanzisha mpango wa kuwapa mawaidha watoto kuhusu athari hasi za kufanya ngono likilenga kuhakikisha wasichana hawapati mimba za mapema.

Akizungumza na Taifa Leo katika mmojawapo wa mkutano uliofanyika katika kanisa la Full Gospel, Magongo eneo la Changamwe, katibu wa kundi linalojiita Life Spring Community, Bi Rose Adiosit alisema kuwa wanaitikia wito uliotolewa na Rais Uhuru Kenyatta katika hotuba yake moja akihimiza hata mashirika yasiokuwa ya serikali na viongozi wa dini wasaidie kurejesha maadili katika jamii.

Hii ni baada ya Rais Kenyatta kutaja kuwa visa vya watoto waliopachikwa mimba wangali wadogo kiumri na visa vingine vya dhuluma za kijinsia vimeongezeka katika kipindi hiki cha janga la corona.

“Tunawapa vijana hao mafunzo kabambe ili waweze kujua athari za kufanya ngono wangali wachanga. Pia, tunaandaa mashindano kama vile ya upishi ili kuwasaidia kupata ujuzi utakaowasaidia baadaye maishani,” akasema Bi Adiosit.

Mshirikishi huyo wa kundi hilo alisema kuwa pia ni muhimu wavulana nao wahusishwe katika mipango hiyo.

“Kuna muda ambapo mvulana pia anaweza kupatikana katika mtego kama vile anampachika msichana mimba, na wote bado hawajakuwa watu wazima kikamilifu. Hivyo, ni vizuri wavulana nao wapewe mafunzo wajiepushe na tabia kama hizo na wajikinge kupata maradhi kama vile Ukimwi na kaswende,” akasema huku akiongeza kuwa wanapanga kufanya mikutano kama hiyo mara mbili kwa wiki, kila Jumatano na Jumamosi, katika maeneo tofauti ya kaunti hiyo.

Baadhi ya wasichana wakishirikiana kuandaa viungo vitakavyotumika katika mapishi. Hawa ni baadhi ya wasichana ambao wanafunzwa kuhusu athari hasi za ngono katika umri mdogo katika mikutano inayofanywa na kundi la vijana linalojiita Life Spring Community. Picha/ Diana Mutheu

Tayari zaidi ya wasichana 20 wenye umri wa miaka 12 hadi 17 wamepata mafunzo hayo.

Mmoja wa waliofaidika na mradi huo, Ann Mwende, 17, alisema wamejifunza mengi na wangependelea hafla nyingi kama hizo ziwe haswa msimu huu ambapo shule zimefungwa.

“Lililobakia ni jukumu langu kufuata mambo niliyofunzwa ili kuepuka mimba kabla ya kuingia utu uzima na kuwa katika ndoa. Pia, nimejifunza jinsi ya kupika,” akasema Mwende.