Habari Mseto

Kunguru kero tupu kwa starehe Pwani wageni wakishindwa kutembea nje

Na MISHI GONGO December 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WADAU wa utalii wa Pwani wanataka kuharakishwa mikakati ya kukabili kunguru ambao wamezidi kuwa wasumbufu hasa katika maeneo ya utalii.

Mpango unaoendelea wa kuwaangamiza katika maeneo ya Kaskazini mwa Pwani kama vile Watamu na Malindi tayari umeua kunguru 94,288, na mizoga yote huwa inakusanywa na kuzikwa ili kuepusha uchafuzi wa fukwe na maeneo ya umma.

Hata hivyo, wadau wa utalii wanasema ndege hao wameongezeka Pwani na kuwa wasumbufu kwa umma. Wadau wa utalii wasema wanataka kuharakisha mpango huo kabla ya Krismasi.

Bw Eric Kinoti Kiambi, mratibu wa mradi wa ‘crows no more’ ulio chini ya shirika la A Rocha Kenya, asema kikosi kinachoshirikiana na Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori nchini (KWS), Bodi ya Kusimamia Bidhaa za Kudhibiti Wadudu na serikali za kaunti husika hutumia dawa ya Starlicide (DRC 1339) kuwaangamiza kwa sababu hulenga kunguru pekee na haiachi sumu kwenye mizoga.

“Kunguru hawa wameongezeka kwa kasi ya kutisha na kuwa tishio kubwa kwa mazingira, afya ya umma na uchumi wa utalii. Tumejizatiti kwa mpango salama, wa kisayansi na wa pamoja wa kuwaangamiza,” Bw Kinoti alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wahudumu wa Hoteli za Pwani Dkt Sam Ikwaye, alisema ndege hao wamezidi kuwavunja moyo wageni wanaokuja kufurahia mandhari ya nje.

“Wageni wanapokuja Pwani, wanataka kufurahia mazingira ya nje lakini wengi hawawezi kwa sababu ya ndege hao,” alisema Dkt Ikwaye.

Dkt Ikwaye alisema wahudumu wa hoteli wanataka Krismasi isiyo na kunguru, akiongeza kuwa, utoaji chambo tayari umeanza Shanzu, Bamburi, Nyali na hadi Tamarind ambako ongezeko la idadi limeonekana katika siku za hivi majuzi.

“Mombasa, tumeweka chambo kwa wiki moja na tumeona idadi ikiongezeka. Baadhi ya hoteli zinasema idadi ya ndege kwenye eneo moja la kulisha imefikia 60. Ili mpango uwe na mafanikio kikanda, lazima tuutekeleze kwa wakati mmoja ili kuzuia ndege kuhama kutoka eneo moja hadi lingine,” alisema.

Dkt Ikwaye alisema sekta hiyo inahitaji angalau Sh10 milioni kutekeleza zoezi hilo na itafanya shughuli ya kuchangisha fedha Desemba 13 katika Fort Jesus.

Aliongeza kuwa, hoteli huwa zinatoa nyama kila siku kusaidia kuweka chambo, lakini gharama bado ni kubwa, kuashiria athari kubwa kiuchumi.

Alisema changamoto ya upatikanaji wa sumu pia ilibainika Kwale, na sumu hiyo huwa ni lazima itumike haraka kabla ya kupoteza nguvu.

Wahudumu wa hoteli walisema mbinu za awali kama kuharibu mayai na viota hazikufanikiwa kwa sababu ndege hujenga viota juu zaidi kwa miti.

Bw Hilary Siele Meneja Mkuu wa Hoteli ya Travellers, alisema ndege hao wamekuwa kero kwa wageni na mzigo wa kifedha kwa hoteli.

“Walikuwa wakichafua magari na hata wageni. Wageni hawakuweza kufurahia mandhari ya nje na tulikuwa tukipata hasara tukijaribu kuwazuia,” alisema, akiongeza kuwa walinzi hotelini huwa na jukumu la ziada la kuwafukuza ndege hao mchana kutwa.