• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Kura yalalama kuhusu wizi, uharibifu wa vifaa vya barabarani

Kura yalalama kuhusu wizi, uharibifu wa vifaa vya barabarani

Na MAGDALENE WANJA

MAMLAKA ya barabara za mijini nchini (Kura) imelalama kuhusu visa vinavyoendelea kuongezeka vya uharibifu na wizi wa ishara na alama za barabarani na nguzo za kandokando mwa barabara.

Mamlaka hiyo imesema kuwa kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, vikingi vya barabarani vya zaidi ya Sh5 milioni vimeibwa na genge la wezi jijini Nairobi.

“Tunakashifu kitendo hicho ambacho ni njia mojawapo ambazo Wakenya wanapoteza mamilioni ya pesa kutokana na wizi huo. Wizi huo pia unahatarisha maisha ya wasafiri kwa kukosa viashiria muhimu,” ilisema taarifa iliyotiwa sahihi na afisa wa mawasiliano wa Kura Bw John Cheboi.

Kulingana na mamlaka hiyo, baadhi ya barabara zilizoathirika zaidi ni pamoja na Thika Superhighway, Outer Ring-Road, Ngong Road na Lang’ata Road.

Mamlaka hiyo ilisema kuwa washukiwa watatu walikamatwa mwishoni mwa wiki jana na walifikishwa mahakamani Jumatatu.

Kura sasa inataka kutekelezwa kwa Sheria kuhusu Bidhaa za Vyuma ya Mwaka 2015 ambayo itapunguza na kudhibiti uuzaji wa chuma.

Hii inajiri mwezi mmoja baada ya mamlaka hiyo kutangaza kuwa itatoa kitita cha Sh100,000 kwa yeyote atakayetoa habari ama kuwaripoti wezi wa vifaa vya barabarani.

You can share this post!

Mpango wa kuimarisha maisha ya vijana wanaorandaranda Nakuru

Habari njema kugundulika kwa kobe adimu Lewa

adminleo