Habari Mseto

KURUNZI YA PWANI: Nitazima genge linalohangaisha wakazi Kisauni – Boinnet

November 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MOHAMED AHMED

GENGE jipya lililozuka katika eneo la Kisauni na kuua watu 10 ndani ya wiki mbili limeanza kuwanyima maafisa wa usalama usingizi.

Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet Jumapili aliungama kuwa kuna shida katika eneo hilo la Kisauni huku akieleza kuwa wanasaka mbinu za kupambana na genge hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kaunti ya Mombasa, Bw Boinnet alisema kuwa licha ya kuwa kuna tatizo eneo hilo sio wakati mwafaka wa kuanzisha kikosi cha polis wa akiba.

Afisa wa usalama eneo hilo pamoja na viongozi wa kisiasa walisema kuwa kutakuwa na haja ya kuwepo kwa askari hao wa akiba iwapo hali hiyo ya kutatanisha haitotatuliwa.

“Ni kweli tuko na shida katika eneo la Kisauni, hilo hatuwezi sema ni uongo lakini azma yetu ni kupambana na genge hilo na kuhakikisha kuwa tunarekebisha uovu huo. Tutapambana na wao kisheria,” akasema Bw Boinnet.

Alipoelezwa kuwa watu 10 wameuawa ndani ya wiki mbili, Bw Boinnet alionekana kushtuka na kumtaka kamanda wa polisi kanda ya Pwani Noah Mwivanda kujibu swali hilo kutoka kwa Taifa Leo.

“Watu kumi? Ndani ya wiki mbili? Na genge hilo hilo? Wacha kamanda wa polisi wa hapa ajibu swali hilo,” akasema Bw Boinnet huku akipinga madai ya polisi kuhusika katika kutoa sare zao kwa wahalifu hao.

Wahalifu hao wameonekana kuvalia sare za polisi wakati wanapotekeleza mashambulizi yao, kulingana na waathiriwa.

Bw Mwivanda kwa upande wake alisema kuwa wapo na taarifa kuhusu genge hilo ambalo wanasema kuwa ndani ya siku mbili wahalifu watakuwa wamekamatwa.

Bw Mwivanda aliongeza kuwa maafisa wa polisi wamekuwa wakifika mahali panaporipotiwa matukio ndani ya dakika 10, na kudai kuwa huenda waathiriwa wanafananisha maafisa na wahuni hao.

“Hiyo ni kwa sababu maafisa wetu hufika mapema na wale ambao wamevamiwa wanadhani kuwa ni polisi ndio waliotekeleza hayo,” akasema Bw Mwivanda.

Ripoti za ndani za ujasusi kutoka kwa polisi zinaeleza kuwa genge hilo jipya lipo na watu kati ya 40 hadi 50 ambao huhangaisha watu wakiwa kati ya watu wawili hadi tano.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa genge hilo linahangaisha maeneo ya Mtopanga, Vikwatani, Ng’ombeni Kajiweni, Mshomoroni, Kadongo, Chembani, SunguSungu na New Hope Primary.

Eneo la Kisauni limekuwa likigonga vichwa vya habari kwa muda sasa kufuatia ongezeko la visa vya uhalifu.

Baada ya maafisa wa usalama kujitahidi kupambana na makundi ya vijana, kundi hili jipya ndio mtihani ambao polisi wanaokodolea macho bila wakitafakari mahali wakapoanzia.

Bw Boinnet alisema kuwa tayari wapo na mipango kabambe ambayo wameweka kuhakikisha kuwa magenge ya wahalifu yanamalizwa.