Habari Mseto

KURUNZI YA PWANI: Wafanyakazi 200 wa makonge sasa watishia kugoma

November 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na LUCY MKANYIKA

ZAIDI ya wafanyikazi 200 wa kampuni ya Makonge ya Voi, Kaunti ya Taita Taveta wametishia kugoma ikiwa hawatalipwa mishahara yao ya miezi sita wanayodai.

Wafanyikazi hao ambao wanafanya kazi katika vitengo mbalimbali vya shamba hilo walisema kuwa mwajiri wao amekuwa akiwanyanyasa bila mshahara na kuwapa ahadi za uongo.

“Tumekaa bila mshahara kwa takriban miezi sita sasa. Kila siku twaahidiwa kuwa tutalipwa lakini hadi leo hakuna mwelekeo,” akasema mmoja wao aliyetaka jina lake libanwe kwa kuogopa maonevu kazini.

Walisema kuwa vilevile wanafanya kazi katika mazingira duni na juhudi za kupata usaidizi katika afisi za Leba za Voi hazijafua dafu.

Walidai kuwa huenda maafisa hao waliingizwa mifukoni na wasimamizi wa kampuni hiyo.

“Kila siku twalalamikia shida zinazotukumba kazini lakini serikali na idara husika haziingilii kati,” akasema mfanyikazi mmoja.

Wiki jana,wafanyikazi hao waliandamana hadi katika afisi za Leba za Voi ili kutoa kilio chao.

Baadaye waliandamana hadi kwa afisi za naibu kamishna wa Voi Bw Joseph Mtile.

Waliahidiwa kuwa serikali itafanya mkutano na usimamizi wa kampuni hiyo hapo kesho (Jumatatu) ili kutafuta suluhu ya shida hiyo.

Wakati huohuo, katibu wa chama cha Cotu katika kaunti hiyo Bw Richard Juma alisema kuwa wafanyikazi hao watagoma ikiwa kampuni hiyo haitasikiza matakwa yao.

Bw Juma alisema kuwa kampuni hiyo inadaiwa mamilioni ya pesa ya mishahara na kusisitiza kuwa lazima walipe deni hilo.

“Tumejaribu sana kuongea na mwenye kampuni alipe wafanyikazi lakini kila wakati anashindwa kutelekeza jinsi tulivyokubaliana,” akasema.

Vilevile alishtumu maafisa wa Leba kwa kushindwa kushughulikia swala hilo kwa haraka ipasavyo.

Wakati huohuo maafisa wa Leba walisema kuwa tayari kampuni hiyo imeahidi kuwa italipa wafanyikazi wake wiki hii.

Shamba hilo ni mojawapo ya kampuni tatu za makonge zilizoko katika kaunti ya Taita Taveta.

Zingine ni Teita (Mwatate) na Taveta iliyoko katika kaunti ndogo ya Taveta ambayo inamilikiwa na aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Bw Basil Criticos.