Habari Mseto

Kusema uongo kulivyomfanya apigwe marufuku kushtaki yeyote

June 15th, 2024 2 min read

Na BRIAN OCHARO

KWA muda wa miaka minane iliyopita, mahakama ya Mombasa imekuwa ikijitahidi kubaini ikiwa mfanyabiashara mmoja kwa jina Julius Odhiambo Oduor alipoteza meno manane au mawili.

Rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa mnamo Januari, 2,2015, Bw Oduor alikuwa akiendesha baiskeli kutoka kwenye kichinjio cha Mikindani akiwa amebeba Kilo 90 za nyama.

Kwa bahati mbaya, inadaiwa alitumbukia kwenye shimo lilokuwa na kina cha futi nne lililochimbwa na kampuni ya Gati Cleaning Agency.

Kampuni hiyo ilikuwa imeagizwa na serikali kukarabati barabara.

Kufuatia ajali hiyo, Bw Oduor alienda kortini mwaka huo huo na kushtaki kampuni hiyo akidai fidia kutokana na majeraha aliyoyapata.

“Shimo liliachwa kando ya barabara kwa uzembe kiasi cha kusababisha hatari kwangu na kwa wananchi wengine,” mwathiriwa aliambia mahakama.

Kulingana na Bw Oduor, alipoteza meno ya chini ya mbele nambari 31 na nambari 34 pamoja na jeraha kwenye paji la uso, mashavu yote na mguuni.

Kuwajibikia kwa ajali

Kampuni hiyo kupitia mkurugenzi wake Jonathan Wepukhulu, ilikanusha kuwajibika kwa ajali hiyo na kuomba mahakama kutupilia mbali madai hayo ya Bw Oduor.

Katika hukumu iliyotolewa Februari 22, 2019, mahakama ya hakimu mkazi ilisema kampuni hiyo inawajibika kwa asilimia 100 kwa ajali hiyo, na ikamlipa Oduor jumla na fidia maalum ya Sh455,000 na 46,400 mtawalia.

Badala ya kulipa fidia, kampuni hiyo iliwasilisha rufaa katika Mahakama Kuu dhidi ya fidia hii, ambapo ilidai kuwa mahakama ya hakimu mkazi ilikosea kisheria.

Katika kipindi cha rufaa hii, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) alituma maombi na kuruhusiwa kushiriki katika rufaa hiyo. Alisema alipata ushahidi mpya ambao angewasilishwa kusaidia mahakama kufikia uamuzi wa haki kwa pande zote mbili.

Jambo jipya lililojitokeza ni kwamba Bw Oduor alikuwa amewasilisha kesi nyingine kadhaa kuhusu ajali hiyo hiyo na uamuzi kutolewa.

Wakati wa kusikizwa kwa rufaa hii, Bw Oduor alihojiwa na ikabainika kuwa alikuwa amejeruhiwa na kupoteza meno sawa katika kesi nyingine kadhaa za awali.

Zaidi ya hayo, mahakama iliamua kwamba Bw Oduor –alifanya kosa kuwasilisha kesi hiyo hiyo katika mahakama kadhaa na kupigwa marufuku kuwasilisha kesi yoyote mahakamani.

“Mwenye kesi hii hatawasilisha kesi yoyote katika Jamhuri ya Kenya dhidi ya mtu au taasisi yoyote bila kibali cha maandishi kutoka kwa Manasheria Mkuu,” mahakama iliamua.

Mnamo 2019, Bw Jonathan aliiandikia Mahakama moja kwamba Bw Odor amekuwa akitoa madai ya uwongo kortini kwa nia ya kuwaibia raia na mashirika yasiyo na hatia.